Na WAF – ARUSHA
Jumla ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia wapatao 49 wamepokelewa mkoani Arusha na uongozi wa mkoa huo kwa ajili ya kambi ya matibabu ya siku sita kwa wilaya zote saba za mkoa huo huku wakitakiwa kuwahudumia wananchi kwa moyo wa upendo.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 21, 2024 na Mganga Mkuu wa mkoa wa Arusha Dkt. Charles Mkombachepa wakati wa hafla ya mapokezi hayo iliyofanyika Hospitali ya mkoa Maount Meru.
“Mtakuwepo kwenye mkoa huu wa kitalii kwa siku sita kuwahudumia wana Arusha, wito wangu kwenu, kaonesheni upendo ili hata mkimaliza kazi yenu majina na kazi yenu ibakie kwenye mioyo ya wana Arusha”. Amesema Dkt. Mkombachepa.
Amesema Rais Dkt. Samia amewaheshimisha watanzania kwa kushusha huduma za kibingwa hadi ngazi ya msingi hivyo ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza.
Akitoa Salam za Wizara, Katibu wa Afya kutoka Wizara ya Afya Rahim Ngaweje, amesema zoezi hilo ni muendelezo wa zoezi la awamu ya kwanza baada ya kupata mafanikio makubwa.
“Baada ya awamu ya kwanza kuwafikia wananchi takribani 70,000, Serikali ikaona ni vema kufanya kwa awamu nyingine, kwani wananchi wengi wenye mahitaji ya kibingwa ilibainika kushindwa kuzifikia huduma kutokana na gharama”. Amesema Rahim.
Ameongeza kuwa, katika zoezi hilo la awamu ya kwanza walibaini baadhi ya watu waliopewa rufaa walirejea nyumbani kutokana na gharama za kumtoa mgonjwa kutoka eneo moja kufikia huduma za kibingwa, hivyo Rais Dkt. Samia akaona ni vema ifanyike kwa awamu nyingine wananchi wengi wafikiwe.
Wakizungumza kwa niaba ya Madaktari Bingwa wenzao Dkt. Patrick Kushoka na Muuguzi Mkunga Fatma Sitta wameonesha utayari wao kwenda kuwahudumia wanaarusha hivyo wajitokeze kwa wingi.
“Moja ya jukumu tulilokabidhiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wenzetu kwenye ngazi ya msingi, hivyo tutawaeleza namna bora yakumhudumia mathaĺani mama anapofika kituo cha afya kujifungua ili asipoteze maisha kwa sababu za uzembe”. Amesema Bi. Fatma.
Madaktari waliopokelewa ni wale wa fani za Meno, usingizi na ganzi salama, upasuaji, magonjwa ya ndani, watoto na wanawake pamoja na wauguzi wakunga Bingwa, ambapo kambi hiyo itadumu kwa siku sita kuanzia Oktoba 21 hadi 26, 2024 kwa mkoa huo.