Na. WAF – Kilimanjaro
Uongozi wa Serikali katika Mkoa wa Kilimanjaro umetoa wito kwa timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia kuwa chachu ya kuleta weledi wa utendaji kazi kwa wataalamu wa afya katika Hospitali za Wilaya za Mkoa huo ili kuhakikisha ubora wa huduma za afya kwa wananchi unapatikana na kuonesha tija ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya nchini.
Wito huo umetolewa na Mganga mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Jairy Khanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa uzinduzi wa kambi ya siku saba ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia watakaotoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika Halmashauri sita za mkoa huo.
“Mbali na kutoa Huduma za kibingwa na bingwa bobezi katika vituo vyetu naombeni mtusaidie kuwakumbusha watumishi wa afya katika vituo mnavyotoa huduma hizi, kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kutumia kauli nzuri kwa wagonjwa wanaowahudumia ili kuleta ubora wa huduma pamoja na tija ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya kwa kufungamanisha huduma za afya na wananchi wa ngazi ya msingi,” amesisitiza Dkt. Khanga.
Ameongeza kuwa Kilimanjaro wanamshukuru Dkt. Samia kwa maono yenye tija ya kuhakikisha wananchi wa ngazi ya msingi wanapata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika maeneo yao na kusaidia wananchi hao kutotumia gharama kubwa kufuata huduma hizo mbali na maeneo yao.
Kwa upande wake Mratibu wa Kambi ya Madaktari Bingwa wa Samia, kutoka Wizara ya Afya, Bi. Jackline Ndanshau amesema kuwa lengo kuu katika kambi hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika Halmashauri zote 184 nchi nzima.
“Serikali imeendelea kuimarisha na kuanzisha wodi maalum za watoto wachanga wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu (NCU) na kutoa mafunzo elekezi kazini kwa watoa huduma za afya, ili kuimarisha ubora wa Huduma za afya katika hospitali zote nchini,”. ameeleza Bi Ndashau.
Aidha, amesema kuwa kila Halmashauri ya Wilaya katika Mkoa wa Kilimanjaro itakuwa na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, daktari bingwa wa watoto na watoto wachanga, daktari wa usingizi na ganzi, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, daktari bingwa wa upasuajhi na mfumo wa mkojo, daktari bingwa wa kinywa na meno na muuguzi bingwa.