Na Grace Semfuko, Maelezo.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, leo Oktoba 21, 2024, imetiliana saini makubaliano ya uwekezaji na mafunzo na Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Kielekroniki ya China (CECIS LTD) ambapo kupitia makubaliano hayo, zaidi ya makampuni 600 ya vifaa vya kompuya yataweza kuwekeza nchini.
Lengo la uwekezaji huo ni kuongeza ujuzi kwa vijana na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utengenezaji wa kompuya kimataifa.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Abdulla na Mwenyekiti wa Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Kielekroniki ya China CECIS Bw. Guo Zhaoping na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Maryprisca Mahundi ambaye amesema Tanzania inakwenda kupiga hatua kubwa katika masuala ya uchumi wa kidijitali.
“Makubaliano haya ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China aliyoifanya hivi karibuni, Kampuni hii ni wabobezi wa masuala ya usalama wa mitandao hivyo elimu waliyonayo itawawezesha vijana kujifunza kwani tunahitaji wataalam wengi zaidi wa TEHAMA nchini” amesema Mhe. Mahundi.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Abdulla amesema uwekezaji huo utatoa fursa kwa watanzania kujifunza na kupata ajira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya huduma za mawasiliano ya kielekroniki ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia wa Kamati ya Kampuni hiyo Bw. Guo Zhaoping amesema uwekezaji huo umefuata misingi ya nchi za Tanzania na China na kwamba unalenga kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
“Kampuni yetu inafanya uwekezaji katika mambo makuu matano ikiwepo sekta ya kompuya na usalama wa mitandao ambapo pamoja na kufanya shughuli za kibiashara pia tunalenga kukuza uchumi wa kidijitali baina yetu na nchi zingine, kwa hapa Tanzania tutafanya kazi kulingana na mahitaji” amesema Bw. Zhaoping.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga amesema pamoja na mambo mengine, pia wamekubaliana kuvutia makampuni mbalimbali ya Kielekroniki kuwekeza nchini ambapo mwaka 2025 kutakuwa na maonesho makubwa ya utengenezaji wa vifaa vya kompuya Afrika ambapo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume yake watakuwa wenyeji wa maonesho hayo.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Abdulla na Mwenyekiti wa Kampuni ya huduma za Mawasiliano ya Kielekroniki ya China (CECIS) Bw. Guo Zhaoping.