*Balozi wa Belarus aeleza utayari wa kubadilishana utaalam wa teknolojia
*Waziri Mavunde aainisha fursa zinazotokana na uwepo wa madini mbalimbali
*Waziri asisitiza umuhimu wa mitambo na teknolojia kwa wachimbaji wadogo
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, leo tarehe 24 Oktoba 2024, amefanya mazungumzo na Balozi wa Belarus nchini Tanzania, Mheshimiwa Pavel Vziatkin. Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, hususan kwenye sekta ya madini, na kubadilishana utaalam wa teknolojia kati ya nchi hizo mbili.
Balozi Pavel alieleza kuwa lengo la ziara yake ni kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi baina ya Belarus na Tanzania. Pia, alionyesha nia ya Belarus katika kushiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini nchini Tanzania, akieleza namna nchi yake ilivyopiga hatua kubwa katika teknolojia na utengenezaji wa mitambo inayoweza kutumika kuboresha uzalishaji wa madini.
Waziri Mavunde alibainisha kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini mbalimbali, ikiwa ni pamoja na madini ya metali, vito, na madini mkakati. Aliwasihi wawekezaji kutoka Belarus kufaidika na fursa hizi, akieleza kuwa nchi hiyo inaendelea kuvutia wawekezaji wa kimataifa kutokana na sera za kuvutia uwekezaji zilizowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia falsafa ya 4R.
Waziri Mavunde pia alisisitiza kuwa Tanzania imepiga marufuku usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi, na hivyo kuwepo kwa nafasi ya kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi. Aliwataka wawekezaji wa Belarus kufikiria kuwekeza katika viwanda hivyo.
Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa, ingawa Tanzania ina wachimbaji wakubwa wanaotumia teknolojia za kisasa, wachimbaji wadogo bado wanatumia zana duni. Alimwomba Balozi Pavel kuangalia uwezekano wa kuzalisha mashine za gharama nafuu ambazo zitasaidia kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo, ambao huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wa madini mkakati, Waziri Mavunde alieleza kuwa Tanzania inatarajia kuanza uzalishaji wa miradi zaidi ya 12 inayohusisha madini haya, hatua itakayoiweka nchi kwenye ramani ya uzalishaji mkubwa wa madini muhimu barani Afrika.
Mwisho, Waziri Mavunde alitumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji na makampuni kutoka Belarus kushiriki katika Mkutano wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC), unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba 2024. Alisisitiza kuwa mkutano huo ni fursa nzuri kwa makampuni ya Belarus kufahamu kwa undani zaidi fursa zilizopo kwenye sekta ya madini nchini Tanzania.