Na Sophia Kingimali.
Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (Tamwa) na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) wameongeza muda kuwasilisha kazi za kushiriki katika tuzo za habari za maendeleo zifahamikazo kama SAMIA KALAMU AWARDS kutoka Oktoba 26 mpaka 30 ambapo washiriki 250 kutoka mikoa 23 wamewasilisha kazi zao kwa ajili ya kushindania tuzo hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 24,2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa Dk.Rose Reuben amesema kazi zilizowasilishwa zimetoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam,Dodoma,Shinyanga,Mwanza,Mtwara,Simiyu,Geita,Njombe,Mbeya,Songwe,Rukwa.
Amesema kutokana na muitikio huo na umuhimu wa tuzo hizo Tamwa na TCRA wameamua kuongeza muda wa kuwasilisha tuzo hizo kutoka Oktoba 26 mpaka 30.
“Uamuzi huu wa kuongeza muda umechukuliwa ili kutoa nafasi kwa wale waliokutana na changamoto za kiufundi, ikiwemo kushindwa kupandisha kazi mitandaoni, kutokana na matatizo ya mtandao na changamoto nyingine.
“Tuzo hizi zitatolewa kwa wanahabari wa Kitanzania, zikiwa na lengo la kuhamasisha, kukuza na kupanua wigo wa uandishi, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani, kupitia vyombo vya habari vya asili na mitandaoni, ili kuchochea andishi wa makala za kina zinazozingatia maendeleo, uwajibikaji, mila na tamaduni pamoja na kujenga chapa na taswira ya nchi yetu,”amesema Dk.Rose.
Amesema hiyo fursa adhimu kwa vyombo vya habari, waandishi wa habari, na maafisa bari kuonesha umahiri wao wa kuchakata habari na kuthaminiwa kwa michango katika taaluma ya uandishi.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa kazi zinazowasilishwa zinatakiwa kuwa za kipekee na ambazo hazijawahi kuwasilishwa kuwania tuzo nyingine, na zinazofuata taratibu za haki miliki. Waandishi wanatakiwa kuwasilisha kazi zao kupitia tovuti rasmi ya www.samiaawards.tz,”amesema Dk.Rose.
“Tuzo za Samia Karamu Awards tumeongeza muda wa kushiriki hadi Oktoba 30 awali ilikuwa Oktoba 26,uamuzi huu umetokana na watu kupambana na changamoto zakimtandao hasa wakati wa wakupandisha kazi.
“Kwa taarifa hii tunawahamasisha wale ambao hawajawasilisha kazi zao kuchukua hatua,kazi zinazowasishwa kuwa zakipekee ambazo hazijawahi kuwaniwa sehemu nyingine,”amesema Dk.Rose.
Amesema mchakato wa upigaji kura
utaanzia kwa wananchi ambapo utaanza rasmi Novemba 8,2024.
“Tunawahimiza wanahabari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika upigaji kura kwa wingi, kwani kura za wananchi zinachangia asilimia 60 ya alama za mshindi, huku asilimia 40 zikiamuliwa na jopo la majaji. Wananchi wataweza kupiga kura kupitia namba maalumu ya SMS SHORT CODE 15200 au kwa kutumia tovuti rasmi,”amesema Dk.Rose.
Naye Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Andrew Kisaka amesema tuzo hizo ni muhimu kwa ajili ya kukuza na kutambua mchango wa waandishi wa habari katika masuala mbalimbali yakiwemo ya maendeleo.
“Tunaamini waandishi wa habari mna michango mizuri kwa jamii kupitia kazi zenu mlizozifanya kwenye redio, televisheni na mitandao ya kijamii. Nawahimiza kuziwasilisha kwa haraka katika kipindi hiki kilichobaki kwani tunaamini zimeleta mabadiliko chanya kwenye jamii,”amesema Mhandisi Kisaka.