Rais wa mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMnet) na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi,akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 25,2024 jijini Dodoma kuhusu Mkutano wa mtandao utakaofanyika kwa siku nne jijini Arusha kuanzia Novemba 4 hadi 7, mwaka huu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Rais wa mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMnet) na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi,akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 25,2024 jijini Dodoma kuhusu Mkutano wa mtandao utakaofanyika kwa siku nne jijini Arusha kuanzia Novemba 4 hadi 7, mwaka huu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Na.Alex Sonna-DODOMA
TANZANIA inatarajiwa kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa tisa wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMnet) utakaofanyika kwa siku nne jijini Arusha kuanzia Novemba 4 hadi 7, mwaka huu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Akizungumza leo Oktoba 25,2024 na waandishi wa habari jijini Dodoma,Rais wa mtandao huo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi, amesema kuwa mkutano huo unatarajia kuwa na washiriki kati ya 400 hadi 500 kutoka barani Afrika.
Amesema kuwa mkutano huo unalenga kuendeleza malengo muhimu ya kimkakati kwa maendeleo endelevu ya usimamizi wa rasilimali watu katika sekta ya umma barani Afrika pamoja na kubadilishana uzoefu na utaalamu ili nchi zipige hatua ya maendeleo kwa kutumia mbinu za kisasa za rasilimali watu.
“Tanzania ikiwa ni mojawapo ya nchi wanachama wa APS-HRMnet imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa tisa wa APS-HRMnet ambao utafanyika tarehe 4-7 Novemba 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) huko Arusha,”amesema
Ameongeza kuwa“Mkutano huu utawakutanisha Mawaziri katika sekta ya umma, Makatibu Wakuu, wanataaluma na wataalamu mbalimbali wa Afrika na kauli mbiu ni ‘Uhimilivu wa utawala na ubunifu kukuza sekta ya umma yenye uelekeo wa baadae kupitia uongozi wa rasilimali watu’ niwaalike wataalamu wote kujisajili kuhudhuria mkutano huu muhimu wa kubadilisha na uzoefu na utaalam,”
Hata hivyo ameeleza kuwa mkutano huo utasaidia kukuza ujifunzaji endelevu, kuongeza maarifa, kuboresha ujuzi, na kuendeleza kizazi cha sasa na kijacho cha wataalamu na viongozi wa usimamizi wa rasilimali watu katika sekta ya umma barani Afrika.
“Mtandao huo una malengo mahsusi ya kubadilishana utaalamu, uzoefu na mbinu za kisasa katika uendeshaji wa rasilimali watu kwenye utumishi wa umma kupitia utafiti na mbinu mbalimbali zinazojitokeza duniani.”amesema
Awali, afafanua historia ya mtandao huo kuwa umetokana na mkutano uliofanyika Eswatini mwaka 2017 wa Mawaziri wa Utumishi wa Umma ambao walikuja na wazo la kuwapo na mtandao ili kusaidia kuharakisha maendeleo barani humo.
“Mtandao huu uliundwa rasmi katika mkutano uliofanyika Arusha na tulipata bahati ulivyoanzishwa Rais wa kwanza alikuwa George Yembesi aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, mtandao ulianzishwa kwa lengo la kutafsiri mikakati ya kimaendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kujenga uwezo wa rasilimali watu yenye matokeo chanya kuhudumia watu barani Afrika,”amesema