Mkutano wa watumishi wa Mungu na waandishi wa habari ukiendelea
Nabii Alpha Kihamba (katika) akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha waandishi wa habari na viongozi wa dini, kusho ni Mtumishi wa Mungu Agness Bruno
Kiongozi wa Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni Mwl.Augustine Tengwa (kulia) akizungumzia suala la kulinda Amani kwenye Mkutano wake na Waandishi wa Habari Jijini Mwanza kushoto ni Nabii Alpha Kihamba.
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Watanzania wameombwa kulinda na kuitunza Tunu ya amani waliyopewa na Mwenyezi Mungu ili kuendelea kuwa na Taifa salama hususani katika kipindi cha uchaguzi.
Ombi hilo lilitolewa leo Jumamosi Oktoba 26, 2024 na Kiongozi wa Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni, Mwl.Augustine Tengwa katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Kata ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza.
Alisema watanzania wanapaswa kujiepusha na viashiria vya uvunjifu wa amani ikiwemo kutengeneza fitina ya kumchafua na kuharibu mwenendo wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan
“Taifa hili lazima libaki na Amani yake kama msingi wake ulivyojengwa na Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere”, alisema Mwl.Tengwa
Kwaupande wake Nabii kutoka Huduma ya Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni, Alpha Kihamba alisema Mungu amekuwa akiwaonesha mambo mbalimbali yanayoweza kutokea katika kipindi cha uchaguzi ambapo ametoa wito kwa Serikali na viongozi wa dini kuchukua hatua mapema.
“Kila mmoja kwa dini na dhehebu lake tumuombe Mungu msamaha ili aweze kutuepusha na majanga mbalimbali yakiwemo ya umwagaji wa damu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ,mashetani yaliyokusudia kuifanya Tanzania imwage damu hayataweza kwasababu watumishi wa Mungu tupo na tutaomba sana”, alisema Kihamba
Naye Mtumishi wa Mungu, Agness Bruno alisema watanzania wasipuuze ujumbe wa manabii hao kwani ni viumbe waliochaguliwa na Mungu kwa ajili ya Taifa la Tanzania.