Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk,Hussein Ali Mwinyi akikata Utepe kuashiria Ufunguzi Soko la Jumbi Wilaya ya Magharibi B Unguja. (PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk,Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mjasiria Mali wa Soko la Jumbi Sabrina Abdalla Ali wakati akitembelea na kununua Bidhaa katika hafla ya Ufunguzi wa Soko hilo Wilaya ya Magharibi B Unguja.
Na Sabiha Khamis Maelezo 27.10.2024
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema zaidi ya Bilion 96 zimetengwa kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali ili kufanya biashara zao vizuri.
Ameyasema hayo wakati akifungua Soko la Jumbi Wilaya ya magharib “B” ikiwa ni shamrashamra za kuelekea miaka minne ya uongozi wa Dkt. Mwinyi akiwa madarakani.
Amesema wafanyabiashara wapatiwe mitaji ili wafanye biashara zao katika mazingira mazuri.
“Matumani yangu ya kuwajengea soko wafanyabiashara ili waweze kuwa na mazingira bora, yametimia” alisema Dkt. Mwinyi.
Amesisitiza kuwekewa kiwango kidogo cha malipo ili waweze kumudu gharama za kulipia
Dkt. Hussein amewanasihi wafanyabiashara hao kulitunza soko hilo kwa kudumisha usafi na kuwadhibiti watakao chafua ili mazingira yaendane na hadhi yake
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Mohamed amesema Wizara itaendelea kutekeleza yale yote watakayoagizwa kwa haraka ili kuiletea nchi maendelea.
Akitoa taarifa ya kitaalam Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum SMZ Issa Mahfoudh Haji, amesema zaidi ya Bilioni 24 zimetumika katika ujenzi wa soko hilo ambalo limekusanya miundombinu ya kisasa ikiwemo cctv camera, vifaa vya kuzimia moto, alama za utambulisho za kumjuulisha sehemu mbali mbali za huduma pamoja na kuzingatia mahitaji ya watu maalum.
Amefahamisha kuwa soko la Jumbi linabeba wafanyabiashara 4000 ambapo watapewa kipaumbele zaidi wafanyabiashara ambao walikuepo tangu soko la zamani ambapo hatua za uhakiki zimekamilika.
Jengo hilo limejengwa na kikosi cha mafunzo Zanzibar kwa kutiliana saini mkataba baina ya kikosi hicho na Baraza la Manispaa Magharib “B” ambapo ujenzi ulianza Novemba 16, 2022 na kulikabidhiwa katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya Magharib “B” Oktoba 10 2024.