Na WAF – Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametoa siku tatu kwa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kurekebisha mashine ya LINAC inayotoa huduma za tiba mionzi kwa wananchi ndani ili wananchi waendelee kupata huduma kama kawaida.
Waziri Mhagama ametoa agizo hilo Oktoba 28, 2024 wakati wa ziara yake ya kushtukiza kwenye Taasisi hiyo kwa lengo la kuona huduma za tiba mionzi zinazotolewa kwa wagonjwa wa saratani.
“Niwapongeze kwa kutengeneza mashine moja ambayo ilipata hitilafu, lakini sambamba na hilo nawaagiza mtengeneze kwa haraka mashine ya LINAC ambayo mmeniambia inasubiri vipuri ili ikifika Alhamisi ya tarehe 31 Oktoba 2024 iwe imeanza kufanya kazi,” amesisitiza Waziri Mhagama.
Akiwa katika ziara hiyo Waziri Mhagama amezungumza pia na wagonjwa waliofika kupata huduma na kuwahakikishia wagonjwa hao kuwa Serikali ipo mbioni kuongeza mashine nyingine ya Tiba mionzi ili kuondoa adha hiyo kabisa.
Waziri Mhagama ametumia fursa hiyo kuwataka wawekezaji binafsi kuendelea kuwekeza Tanzania kwenye sekta ya afya hususani katika eneo la huduma za tiba mionzi ili kuhakikisha huduma hizio zinakuwa toshelevu.
Aidha, Waziri Mhagama amewasihi Watanzania wote kuendelea kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili pindi wanapopata changamoto za afya wapate huduma za afya bila kikwazo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Julius Mwaiselage ameishukuru Serikali kwa kufanya mchakato wa kuongeza mashine nyingine ya tiba mionzi itakayo saidiana na zilizopo.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kufanya uamuzi mzuri wa kutuongezea mashine nyingine mpya ya huduma za tiba mionzi, hii itasaidia sana kwa kuwa tumekuwa na wananchi wenye kuhitaji huduma hii,” ameshukuru Dkt. Mwaiselage.