*Kutoa mikopo ya simu, bima za aina mbalimbali na mafuta kwa madereva, ili kuwawezesha kutoa huduma bora zaidi
Dar es Salaam – 29/10/2024,
Vodacom Tanzania Plc imetangaza ushirikiano wa kimkakati na Bolt, moja kati ya makampuni makubwa ya teksi mtandao, wakitoa huduma za usafiri nchini, kwa lengo la kuongeza ujumuishwaji wa kifedha kwa madereva na kukuza malipo ya kidijitali. Ushirikiano huu utaleta huduma za miamala ya kifedha kidijitali kwa madereva wa Bolt, wakiwemo madereva wa Magari, Bajaj na Bodaboda, kupitia mfumo wa M-Pesa kutoka Vodacom.
Ushirikiano huu utatoa fursa za kipekee kama mfumo wa malipo bila kutumia fedha taslimu wa ‘Lipa kwa Simu’, mikopo ya simu, aina mbalimbali za bima, mikopo ya wafanyabiashara na mkopo wa mafuta wa Chomoka, iliyotengenezwa mahsusi ili kuwawezesha madereva wa Bolt kutumia fedha zao kiusalama na kwa faida. Huduma hizi zitawarahisishia madereva utaratibu wa malipo na pia kuwasaidia kupata huduma muhimu kama vile matengenezo ya magari, mafuta na bima za vyombo vya moto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania, Epimack Mbeteni, alisema, “Ushirikiano huu unaleta mabadiliko makubwa kwa madereva na wateja pia. Kupitia Lipa kwa Simu, tunawawezesha madereva wa Bolt kutumia mfumo salama, rahisi, na usio wa malipo ya fedha taslimu ambao utawawezesha kuongeza kipato chao na kupata huduma muhimu kama mikopo ya mafuta na bima za aina mbalimbali. Hatua hii ni sehemu ya jitihada zetu za kujenga mfumo thabiti wa malipo bila fedha taslimu na kukuza ujumuishwaji wa kifedha hapa nchini.”
Naye Meneja Mkuu wa Bolt, Dimmy Kanyankole, alibainisha faida za ushirikiano huu kwa madereva na wateja wa Bolt, “tunafurahi kushirikiana na Vodacom Tanzania Plc kwa kuunganisha huduma za M-Pesa na huduma za usafiri wa Bolt. Ushirikiano huu utafanikisha mchakato wa malipo kuwa rahisi zaidi kwa madereva wetu na wateja, huku pia tukitoa huduma za ziada za kifedha zinazosaidia kuinua Uchumi wa madereva. Tunaamini ushirikiano huu utaimarisha sana ustawi wa madereva wetu na kuboresha huduma kwa watumiaji wa Bolt nchini Tanzania.”
Kupitia ushirikiano huu, Vodacom Tanzania na Bolt wanakusudia kuongeza thamani na idadi ya miamala ya kidijitali huku wakipanua wigo wa huduma za kifedha kwa madereva wa Bolt na jamii kwa ujumla. Kwa kutoa mikopo, bima na kurahisisha huduma za malipo, ushirikiano huu unaunga mkono uwezeshaji wa kidijitali na kiuchumi kwa Watanzania.