Na: Dk. Reubeni Lumbagala.
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kusisitiza kuwa juhudi zinazofanywa na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ni lazima ziguse maisha ya watu. Akasisitiza kuwa maendeleo yasiyogusa maisha ya watu hayana maana, ni lazima maendeleo yaguse maisha ya wananachi, kwani hayo ndiyo maendeleo yenye maana, maendeleo ya watu.
Maendeleo ya watu yanaambatana na utekelezaji na uboreshaji wa miradi ya maendeleo. Miradi ya maendeleo kama vile shule, vyuo, hospitali, maji, umeme, barabara, ofisi, masoko, mabwawa na mingine kadha wa kadha inapotekelezwa kikamilifu, inagusa maisha ya watu hasa katika kuboresha maisha ya wananchi ambapo uwepo wa miradi hiyo huleta manufaa katika maisha.
Kimsingi, serikali inawajibika moja kwa moja katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu, serikali inayo wajibu wa kuleta ustawi katika maisha ya wanachi wake.Njia mojawapo ya kuleta ustawi katika maisha ya wananchi ni kuibua miradi ya kimkakati na miradi mingine ili kwa pamoja wananchi wanufaike na hivyo ustawi wa maisha ya wananchi uwe ni halisi.
Miongoni mwa jambo ambalo limepewa msukumo mkubwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (Public and Private Partnership – PPP). Ndiyo maana Januari 5, 2022, Rais Dk. Samia alimteua David Kafulila kuwa Kamishna wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, ili kuwe na msukumo wa kipekee katika ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuchagiza miradi ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi.
Ni katika ushirikiano huu ambao kwa kiasi kikubwa serikali imepunguziwa mzigo katika kuboresha maisha ya wananchi kwani sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa nchi.Ni ukweli ulio dhahiri kuwa ujenzi wa nchi unahitaji juhudi za pamoja.
Ni bahati mbaya wakati mwingine baadhi ya wananchi wamekuwa na dhana potofu kwa kudhani serikali peke yake ndiyo yenye wajibu wa kufanya kila kitu bila kujua kuwa hata mtu binafsi, kampuni, taasisi zisizo za kiserikali, asasi za kiraia nao ni sehemu katika ujenzi wa nchi yaani wanapaswa kushirikiana na serikali katika kutatua kero za wananchi kwa kuibua miradi ya maendeleo yenye tija katika maisha ya wananchi.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa miradi ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi inaibuliwa ili kutatua kero za wananchi badala ya kutegemea na kusubiria fedha kutoka serikalini kutatua kero za wananchi.Sekta binafsi ni mdau muhimu wa maendeleo, na pale kunapokuwa na sekta binafsi imara, kasi ya maendeleo nayo inakuwa kubwa na hivyo maisha ya wananchi yanakuwa bora zaidi.
Kunahitajika uzoefu, utaalamu na raslimali fedha za kutosha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hivyo basi, serikali peke yake inalemewa, na hivyo, ubia kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu sana ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
CHUO CHA CBE MFANO WA KUIGWA MRADI WA UBIA.
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia wa Sekta za Umma na Binafsi (PPP) wameshirikiana ili kufanikisha azma ya kujenga mabweni ya wanafunzi kwa ubia utakaogharimu shilingi bilioni 20.7.
Itaendelea kesho.
Mwandishi ni Mwalimu wa Sekondari ya Mlali ya mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.