Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina aliutaka ulimwengu Jumatano kuliokoa dhidi ya marufuku ya Israel ambayo itakuwa na “matokeo mabaya” kwa mamilioni ya watu walionaswa katika vita huko Gaza.
Philippe Lazzarini, anayeongoza shirika hilo linalojulikana kwa jina la UNRWA, aliambia mataifa 193 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba lazima wachukue hatua ili kuizuia Israel kutekeleza sheria inayokataza shughuli za shirika hilo katika maeneo ya Palestina. Sheria hizo, zilizopitishwa na bunge la Israel mwezi uliopita, zinaanza kutumika ndani ya siku 90.
UNRWA ilianzishwa na Baraza Kuu mwaka 1949 ili kutoa afueni kwa Wapalestina waliokimbia au kufukuzwa makwao kabla na wakati wa vita vya Waarabu na Waisraeli vya mwaka 1948 vilivyofuatia kuanzishwa kwa Israel, pamoja na vizazi vyao, hadi kutakapopatikana suluhu la kisiasa kwa Mzozo wa Israel na Palestina.
UNRWA imekuwa wakala mkuu wa kusambaza misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, ambapo karibu wakazi wote wa Wapalestina milioni 2.3 wanategemea misaada ili kujinusuru wakati wa vita vya zaidi ya mwaka mmoja vya Israel na Hamas. Wataalamu wanasema njaa imekithiri.
The post UNRWA,yahimiza ulimwengu kuiokoa kutoka kwenye marufuku ya Israeli first appeared on Millard Ayo.