Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV.
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua mkutano wa Kimataifa wa wahasibu wakuu wa Serikali kutoka nchi 57 barani Afrika unaotarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 2 hadi Disemba 5 mwaka 2024 Jijini Arusha.
Akizungumza mkoani Morogoro leo Novemba 7,2024 wakati wa semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha,Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA Leornad John Mkude,amesema nchi imepata fursa na bahati kubwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa pili wa Wahasibu wakuu wa Serikali wa Afrika – African Association of Accountants Generals (AAAGs}
“Mkutano wa AAAGs unafanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake Julai 5 mwaka ,2023.Mara ya kwanza ulifanyika nchini Lesotho Februari 2024 na mkutano unaofuata unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa AICC Mkoani Arusha.
“Lengo la mkutano ni Kujenga imani ya umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu,ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha wahasibu wote Tanzania, pamoja na kada zenye uhusiano wa karibu na uhasibu kama, Wakaguzi wa hesabu na maofisa ugavi ili kujenga misingi bora ya usimamizi wa fedha na mali za umma,”amesema.
CPA Mkude amesema Wizara ya Fedha imebaini kuwa mkutano huo ni muhimu katika kukuza utalii wa Mikutano na Matukio (MICE Tourism) pamoja na kutangaza utalii kimataifa,hivyo washiriki watakaohudhuria Mkutano huo watapata fursa ya kutembelea hifadhi mbalimbaki na kutangaza vivutio vilivyopo katika nchi zao.
Ameongeza kuwa wanatarajia wageni kutoka nje kuja nchini na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa Tanzania katika kuunga mkono dhamira ya Rais ya kuutangaza utalii nchini Tanzania.
“Wageni hawa watatembezwa kwenye mbuga za wanyama na vivutio vya utalii na washiriki wa mkutano watatembelea vivutio vyetu vya utalii vya Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Tarangire, Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Duluti, Hifadhi ya Taifa ya Arusha na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro,”amesema CPA Mkude.
Aidha amesema mkutano huo pia utahudhuriwa na Rais wa IMF, PAFA na washirika wa maendeleo wa kimataifa huku ada ya ushiriki ya mkutano ikitajwa kuwa ni Sh.1,300,000, kwa kila mshiriki.
Hivyo amewaomba Wahasibu , Wakaguzi wa hesabu, Maofisa ugavi na Maofisa TEHAMA na wadau wengine hususani watanzania kujitokeza kwa wingi kujisajili kuhudhuria Mkutano huo.
Aidha amesema kuwa Umoja wa Wahasibu Wakuu wa Serikali wa Afrika ulizinduliwa rasmi Mombasa, Kenya Julai 5 mwaka 2023 baada ya azimio la kufunga umoja wa wahasibu wakuu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika (ESAAG) pamoja na Jumuiya nyingine za Wahasibu Wakuu wa Serikali Afrika.
Kwa mujibu wa CPA Mkude ni kwamba kwa sasa nchi 57 za Umoja wa Afrika ni mwanachama wa Umoja huo.Hivyo kufanyika kwa mkutano huo nchini kunakwenda kuongeza na kufungua fursa mbalimbali kwa wahasibu hao ambao pia wakati wa mkutano huo watabadilishana uzoefu wa masuala mbalimbaki ya fedha.
Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA,Leornad John Mkude akizungumza mkoani Morogoro leo Novemba 7,2024 wakati wa semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, ikiwemo taarifa iliyohusu ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa wahasibu wakuu wa Serikali utakaofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,kutoka nchi 57 barani Afrika unaotarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 2 hadi Disemba 5 mwaka 2024 Jijini Arusha .
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wizara ya Fedha,Benny Mwaipaja akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kufungua semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini iliyoandaliwa na wizara hiyo,mkoani Morogoro leo Novemba 7,2024