RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amefungua rasmi ofisi ya wakala wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) iliyopo maeneo ya Minhang, jengo la Ling Hang Group, Shanghai.
Katika hafla hiyo fupi ya ufunguzi rasmi wa ofisi iliyofanyika leo Novemba 07, 2024 Shanghai, China, Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa Zanzibar bado inahitaji wawekezaji katika sekta mbalimbali ili kuimarisha na kukuza uchumi wake. Amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Dk. Mwinyi ameongeza kuwa Serikali ya Zanzibar imedhamiria kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, kilimo, uvuvi, na viwanda ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Kufunguliwa kwa ofisi hiyo ni hatua muhimu ya kufanikisha malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hususan kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya Zanzibar na mataifa mengine.