Happy Lazaro,Arusha
HAKIMU Mfawidhi wa Mahakama ya hakimu Mkazi Arusha, Erasto Philly ameutaka upande wa Mashtaka kuhakikisha upelelezi unakamilika kwa wakati katika kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili Mwekezaji na Mfanyabiashara Saleh Salim Alamry(54) pamoja na wakili wa kujitegemea Shecky Mfinanga .
Aidha Hakimu mfawidhi ameyasema hayo baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama hiyo kwamba upelelezi wa shauri hilo upo mbioni kukamilika ndani ya wiki moja.
Amesema kuwa, ni vizuri upande wa mashatka ukamilishe upelelezi kwa wakati na kuhakikisha haki inatendeka na wakamilishe upelelezi ndani ya wiki mbili ili haki itendeke maana anashindwa kufanya shughuli zake nyingine.
“Upelelezi ufike kwa wakati ili waweze kuendelea na shauri hilo hivyo naomba upande wa mashtaka ifikapo tarehe hiyo muwe mmemaliza upelelezi “amesema Hakimu Mfawidhi.
Mwekezaji Saleh anashikiliwa katika mahabusu ya gereza Kuu la Arusha,Kisongo, kwa zaidi ya siku 80 tangu alipokamatwa agosti 22 mwaka huu,akikabiliwa na makosa 27 yakiwemo ya uhujumu uchumi ,utakatishaji wa fedha na kuongoza genge la uhalifu na kusababisha hasara ya dola milioni 26 ,ambapo mshtakiwa mwenzake Mfinanga yupo nje kwa dhamana.
Hatua hiyo imekuja kufuatia wakili wa serikali Mahfudh Mbagwa kudai mbele ya mahakama ya hakimu Mkazi Arusha kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika na kuahidi kukamilisha ndani ya wiki moja.
Wakili Mbagwa aliiambia mahakama hiyo kwamba baada ya wiki moja upelelezi utakuwa umekamilika, hivyo akaomba tarehe nyingine ya kutajwa wakati jitihada za kukamilisha upelelezi zikiendelea”.
Awali jopo la mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na wakili Faisal Rukaka na wenzake Moses Mahuna, Denis Mworia na Kerry Mra ,wakili Rukaka wamesema wamesikia upande wa Jamhuri wakisema upelelezi bado ila wanatarajia wiki ijayo wawe wamekamilisha , Pia katika muktadha huo waliomba ofisi ya DPP itoe consent kwa Mahakama hii(hati au ruhusa au mamlaka) ili isikilize kesi hii na kutoa baadhi ya amri .
“Pia tunaomba suala hili la upelelezi lifanyike kwa haraka kwa sababu kosa la mteja wetu halina dhamana anakosa kufanya shughuli zake za kila siku.” aliieleza Mahakama.
“Wasipokamilisha upelelezi haraka watakuwa wanaitumia mahakama kama ngazi ya kumtesa mtuhumiwa ,upande wa mashtaka hakikisheni upelelezi unakamilika haraka sio kila siku kuja kusema upelelezi haujakamilika”.
“Kuna nafuu tatu ambazo mnaweza kuzitumia ambazo ni kuipa mahakama hii mamlaka ya kusikiliza shauri hili, kulipeleka Mahakama Kuu au kuwaachia huru watuhumiwa (NOLLE PROSEQUI). Ni vema waendesha mashitaka mkafanya mawasiliano na wapelelezi kuliko kuja kuwasemea wao hapa”ameonya hakimu
Baada ya maelezo hayo hakimu Philly aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21 Mwaka huu itakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa .