Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO)Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga akizungumza Novemba 9,2024 wakati kufungua Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Tanesco Saccos mkoani Dodoma.
Na Mwandishi wetu, Dodoma
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO)Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga ,amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo nchini,kuhamasika kujiunga na Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Tanesco Saccos kwa lengo la kujiwekea akiba itakayoweza kuja kuwasaidia baadae.
Pia amekiahidi Chama hicho kuwa makato yanayotakiwa kukatwa kwa wafanyakazi wa shirika hilo ambao ni wanachama kuingizwa kwenye Tanesco Saccoss amewahaidi kuwasilishwa kwa wakati.
Akizungumza Novemba 9,2024 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 56 wa Chama cha Tanesco Saccos mkoani Dodoma,Mhandisi Hanga amesema utendaji wa Chama hicho umeweza kuimarika zaidi kutokana na mtaji wa chama na mikopo kwa wanachama imeongezeka licha ya changamoto ya kupungua kwa idadi ya wanachama.
Amesema mbali na hilo pia Chama hicho kimeweza kuongeza faida yake ukilinganisha na mwaka ulioisha wa 2022 kufanya chama kuwa na mafanikio makubwa ya kujivunia kwani ni dhahiri kwamba ubora wa huduma ndio uliopelekea kukua kwa mafanikio hayo.
”Napenda kukipongeza Chama hiki cha Tanesco Saccos namna mnavyotekeleza kwa vitendo msingi wa saba wa ushirika wakuijali jamii kwa kuchapisha mashuka 1750 mwaka 2023 -2024 kwaajili ya kutoa msaada kwenye hospitali za mikoa saba kwa lengo la kuzifikia hospitali zote nchini.
”Huu ni upendo wa dhati,naomba msiishie kutoa mashuka tu bali kwenye mahitaji mengine kwa kadri mtakavyojaliwa,”amesisitiza.
Aidha amesema umoja huo wa Tanesco Saccos unajumla ya wananchama kufikia takribani 2000,ambayo ni idadi kubwa na katika vyama vya ushirika nchini saccos hiyo inashika namba nne huku mtaji kufikia Bilioni 71.
”Nasisitiza kuwa bodi iendelee kutekeleza malengo ya mpango mkakati ya chama ikiwa ni pamoja na kusisitiza matumizi mapya ya Akaunti ya Mafao inayolenga kumuwekea mazingira bora ya kustaafu kwa mwanachama sambamba na kukuza ukwasi wa chama huku ikijenga ustahimilivu wa utoaji wa huduma,”amesema.
Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Tanesco Saccos,Hilary Andrea amesema mikopo inayotolewa na Tanesco Saccos kwa wanachama wao inajitahidi kutolewa kwa wakati hasa ile yenye uhitaji wa haraka.
Amesema lengo lao kubwa wanaloliangalia katika chama chao ni kuwepo kwa mikopo ya masharti isiyoumiza ambapo itaweza kufikia kuwa mikopo digiti moja asilimia isiyozidi 12.
”Tumefanikiwa katika mikopo midogo ndani ya muda kadhaa kama miaka mitatu au minne tunatarajia kufikia mikopo mikubwa kuanza kuitoa,”amesisitiza.
Aidha amesema Tanesco saccos ipo katika mfumo unaoratibiwa na benki kuu wa kuwasilisha taarifa za wakopaji wabaya hivyo endapo kunatokea mtu ambaye ni mkopaji mbaya hawawezi kumpatia mkopo.