Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Oktoba 17, 2024, amehitimisha rasmi Mkutano Mkuu wa 149 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (CICG) mjini Geneva, Uswisi.
Mkutano huo umejadili mada kuu inayohusu “Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa ajili ya mustakabali wa Amani na Uendelevu”. Aidha, Mkutano wa 149 umepitisha maazimio kadhaa yanayolenga kurejesha amani katika maeneo yenye migogoro duniani kwa kutumia njia za majadiliano ya kidiplomasia.
Maazimio hayo pia yamejumuisha matumizi ya akili mnemba (AI) katika kuimarisha demokrasia, haki za binadamu na maamuzi ya kisheria, pamoja na rasimu ya mabadiliko ya sheria za uendeshaji wa Baraza la Uongozi na Mkutano Mkuu wa IPU.