Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Haroon Nyongo, akizungumza katika mkutano wa Asasi za Kiraia (AZAKI) uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Januari 10, 2025.

Baadhi ya wana Asasi za Kiraia (AZAKI) wakiwa katika mkutano wa kukusanya maoni ya dira ya maendeleo ya 2050.
SERIKALI ipo tayari kusikiliza maoni ya kila mmoja ili kuhakikisha Dira ya maendeleo ya taifa 2050 inakuwa halisi na shirikishi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Januari 10, 2025 Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, amesema wakati akifungua mkutano wa Asasi za kiraia uliolenga kutoa maoni ya dira ya Maendeleo ya taifa 2050 ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.
Akizungumza katika mkutano wa Asasi za Kiraia (AZAKI) Nyongo amesema kuwa, ni muhimu kuwepo na majadiliano ya pamoja baina ya Serikali na wadau wa maendeleo badala ya ukosoaji ili kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inakua shirikishi.
“Maoni ya wananchi na wadau mbalimbali katika uandaaji wa dira hii ni muhimu kwani yatakuwa msingi wa kuandaa dira hiyo.”Amesema Nyongo.
Aidha,mesema uzoefu wake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii ulimsaidia kuelewa dhamira ya AZAKI katika kutoa maoni yanayolenga kuimarisha maendeleo ya taifa.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge ameainisha kuwa kukuza uchumi shindani ndani ya mikoa ni njia muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu, akitolea mfano wa nchi ya Kenya ambako kaunti zinashindana kwa vigezo vya kuzalisha ajira na kujumuisha makundi ya pembezoni.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuwajumuisha wadau wa kiraia katika uandishi wa Dira ya Maendeleo ya taifa ya mwaka 2050.
Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Lucas Kifyasi, ameongeza kuwa utekelezaji wa dira hiyo utahitaji kipaumbele katika elimu, hasa kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda yanayotarajiwa kuimarika miaka 25 ijayo. Alisisitiza kuwa elimu na teknolojia ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu.
Mkutano huo umeonyesha dhamira ya pamoja kati ya serikali, AZAKI, na wadau wa kimataifa katika kuhakikisha Tanzania inafanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.