Na Nihifadhi Abdulla, Zanzibar
DIRA ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020-2025 katika maadhimio namba 2.5.1 mpaka 2.5.9 yameeleza jinsi gani masuala mbalimbali ya usawa wa jinisia na kuondoa unyanyasaji wa jinsia pamoja na kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wanawake ikiwemo kuinua na kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake katika jamii na kuongeza fursa ya kuwawezesha katika vyombo vya utoaji wa maamuzi katika shughuli za uchumi, kijamii na kisiasa katika ngazi zote za utawala, huduma na sheria
Aidha Katiba ya Zanzibar 1984, katika kifungu 21 (2) kinaelelza kuwa kila mzanzibar anayohaki na uhuru wa kushiriki kikamilifu katika kufikia uwamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke na taifa lake.
Kwa kutambua umuhimu wa mwanamke Sera na Sheria mbalimbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika democrasia ya uongozi sera ya sheria hizo ni pamoja na katiba ya Zanzibar, dira ya zanzibar ya 2020, mkakati wa kupunguza umasikini na kukuza uchumi, sera ya jinsia ya zanzibar, sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.
Licha ya jitihada hizo suala la kuzingatia usawa wa kijinsia Zanzibar nafasi ya viongozi wa Serikali za Mitaa (MASHEHA) inadaiwa kuwa bado nguvu za ziada zinahitajika kuhakikisha inafikiwa asilimia 50kwa 50 huku ikilinganishwa na Idadi ya watu Zanzibar kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022 ambayo jumla ni 1,889,773. Wanaume ni 915,492 sawa na asilimia 48% na Wanawake ambao ni 974,281. Ni sawa na asilimia 52%.
Kwa mujibu wa Idara ya uratibu Tawala za Mikoa Serikali za mitaa Zanzibar Mkoa mjini magharibi ambao una jumla ya wakaazi 893,169 wanaume 427,927 na wanawake 465,242, una shehia 121 masheha wanaume 101 sawa na asilimia 83% na wanawake 20 sawa na asilimia 17% huku Mkoa Kaskazini Unguja ukiwa na jumla ya wakaazi 257,290 wanaume 126,341na wanawake 130,949 una jumla ya masheha 75 kati ya hao wanaume 66 sawa na asilimia 88% na wanawake 9 sawa na asilimia 12%.
Aidha Mkoa wa Kusini Unguja ambao una Shehia 63 masheha wanaume 50 sawa na asilimia 79% na wanawake 13 sawa na asilimia 21% .
Kwa upande wa Mkoa kaskazini Pemba kuna shehia ni 61 masheha wanaume 41 sawa na asilimia 67 na wanawake 20 asilimia 33 na Mkoa Kusini Pemba huu una shehia 68 masheha wanaume 51 sawa na asilimia 75 na wanawake 17 ambayo ni asilimia 25
Kwa ujumla Unguja kuna shehia 259 masheha wanaume 217 sawa na asilimia 84 na asilimia 16 ni wanawake ambao ni 42 Na kwa kisiwa cha Pemba kuna jumla ya shehia 129 masheha wanaume 92 sawa na asilimia 71 wanawake 37 asilimia 29.
Hivyo mchanganuo huu unaeleza kwamba Zanzibar kuna shehia 388 masheha wanaume 309 ambayo ni sawa na asilimia 80 na wanawake 79 sawa na asilimia 20.
Mjumbe wa kamati za siasa Idi chum wa Tunguu anasema katika kumchagua kiongozi nafasi ya usheha mchakato wake haupitishwi na mtu mmoja “ wakati wa kuteua tunaangalia vigezo vingi mfano kiwango cha elimu, kaitumikia vipi jamii na kuishi kwake katika Shehia kuna mchango wowote pamoja na uchangamfu kwa watu”amesema Idi.
Wananchi wanasemaje?
Salama Hussein mkaazi wa Amani anasema suala la uwepo wa sheha wanawake kidogo halipaswi kufumbiwa macho kwani tafiti zinaonesha wanawake wanafanya kazi vizuri zaidi “mimi ninaomba Serikali kuliangalia suala hilo kwa kina wanawake na sisi tupewe nafasi ili tufikie huo usawa wa kijinsia asilimia hii ilokwepo haijatutendea haki kwakweli” amesema Salama.
Ramadhan Piro mwanachi wa Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja anasema “kutokanana wakati uliopo ni vyema nafasi hizi kutotolewa kisiasa lakini kuangaliwa nani mbora na atakae weza kuitumikia jamii yake kwa kuzingatia haki”anasema Piro.
Maburuki Ali Mcha mwanachi wa Magomeni anasema anaimani na viongozi wanawake kuwa wanafanya kazi nzuri “kwa vile hawapati nafasi wanayoitaka basi na masheha wachukue fomu wajinadi ikisha tuwapigie kura kama viongozi wengine mbona wenzetu wanaweza na sisi Zanzibar inawezekana kufanya hivyo”amesema Maburuki
Mkurugenzi Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar Dk Mzuri Issa amesema “Licha ya hayo yote lakini bado hali ya utekelezaji wa sera na sheria hizo hauridhishi na ni kinyume na ilivyoridhiwa mikataba ya kimataifa kwani takwimu za nafasi ya mwanamke uongozi wa usheha kwa Zanzibar nzima yaani Unguja na Pemba ni asilimia 20 tu”amesema Dk Mzuri.
Amesema ili haki ya mwanamke ipatikane ni wajibu kwa Serikali ya Zanzibar ambayo imo ndani ya Tanzania kutekeleza makubaliano ya mikataba mbalimbali inayolenga kuwepo usawa wa kijinsia kwenye nafasi za uongozi.
Azimio la 1325 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilotolewa Tarehe 31 oktoba mwaka 2000 limesema kuongeza ushiriki wa mwanamke katika ngazi za maamuzi inazidisha demokrasia ya nchi, uchumi, amani na utulivu kwa muda mrefu hivyo azimio limezitaka nchi wanachama kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi zote za maamuzi.
Mkurugenzi idara ya uratibu Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa Zanzibar Bi Zainab Khamis Kibwana amesema suala la uteuzi wa masheha lipo kwa mujibu wa Katiba na kusimamiwa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, na kukiri uwepo wa masheha kidogo wanawake ambapo ameeleza kuwa unaotokana na sababu mbalimbali.
“Serikali inajitahidi kuzingatia usawa wa kijinsia kwa mfano hivi sasa masheha wanawake ni kidogo hii inachangiwa na mambo tofauti ikiwemo kiimani na kubwa wanawake wengine bado wanahofu ya kuongoza,
“lakini nichukue fursa hii kuwataka wanawake kutoogopa kurogwa bali wajiamini na waheshimu uteuzi hii ndio njia itakayotufanya tufikie hilo lengo la usawa wa kijinsia” amesema Zainab.