
Kaimu Katibu Mkuu, Activista Tanzania, Erickson Duke akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 08, 2025 kuhusiana na kupinga machafuko ya amani Goma nchini Kongo. 

Baadhi ya wafanyakazi waJukwaa la Vijana la ctivista Tanzania akipingana na vita nchini Kongo.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
JUKWAA la vijana la Activista Tanzania linatoa wito kwa nchi za Afika Mashariki pamoja na nchi za (EAC) na nchi Wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zichukue jukumu madhubuti litakaloratibu kutatua mgogoro unaoendelea Goma huku nchini Kongo.
Kaimu Katibu Mkuu, Activista Tanzania, Erickson Duke ametoa rai hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 08, 2025, amesema kuwa ili kuweza kumaliza Vita nchini Kongo na kueneza amani katika nchi hiyo, viongozi wa Afrika wanapaswa kuweka maslahi ya watu wa Kongo mbele badala ya kushindana kwa maslahi ya kisiasa na kiuchumi.
Duke ameeleza kuwa Mkutano uliopendekezwa wa EAC-SADC unaofanyika jijini Dar es Salaam leo unapaswa kuharakishwa na kutoa ramani ya wazi ya kufanikisha amani na usalama, kuhakikisha kwamba ukanda wa Maziwa Makuu unakuwa salama.
Amesema katika mchakato wa amani ujumuishwe kwa wadau wote wa serikali ya DRC, makundi yenye silaha, asasi za kiraia, wanawake na vijana: Sauti za watu wa Kongo, hasa wale walioathirika moja kwa moja na mgogoro, lazima ziwe kitovu cha mazungumzo yoyote kwa ajili ya maridhiano ya kweli.
“Uchimbaji haramu wa rasilimali za Kongo ukomeshwe mataifa ya Afrika na jumuiya ya kimataifa lazima ziwe na udhibiti mkali wa biashara ya madini yanayotokana na migogoro na kuhakikisha kuwa utajiri wa Kongo unawanufaisha wananchi wake. Maendeleo ya kiuchumi na ajira ni nguzo muhimu kwa amani ya kudumu katika nchi hiyo.” Amesema
Pia jukwaa hilo limeomba misaada ya ya kibinadamu iwafikie wahanga eneo la machafuko ambapo wahusika ni wanawake na watoto wapate huduma za msingi na mhimu, kama maji chakula, malazi na huduma za afya ikiwa na jitihada za makusudi zikifanyika kuleta suluhisho la kudumu la usitishaji wa vita katika eneo la Goma.
“Afrika haiwezi tena kuvumilia mateso ya watu wa Kongo. DRC si nchi tu; ni moyo wa Afrika, yenye utajiri wa utamaduni, rasilimali, na fursa. Mgogoro huu unaoendelea ni usaliti kwa ndoto ya Umoja wa Afrika ya mshikamano, amani, na ustawi wa pamoja.” Amesema Duke
Aidha Duke ametoa rai kwa Makundi yote yenye silaha yaweke chini silaha mara moja na jumuiya ya kimataifa ihakikishe ulinzi wa raia, Umoja wa Afrika (AU) unapaswa kuimarisha ujumbe wake wa kulinda amani kwa mamlaka wazi ya kupokonya silaha wanamgambo na kuwawajibisha wahusika wa uhalifu.
Pia ameomba viongozi wa Kiafrika, hususan ndani ya EAC na SADC, wanapaswa kuonyesha dhamira ya kweli ya kisiasa kumaliza mgogoro huo huku akisisitiza kuwa wakati wa ahadi zisizotekelezwa umepita na kueleza kuwa wakati wa kuchukua hatua ni sasa.
Akizungumzia kuhusiana na watu wa DRC, Duke amesema kuwa uvumilivu wa watu wa DRC ni msukumo kwa dunia…. “Tunasimama nanyi katika harakati zenu za kudai amani, haki, na hadhi, pamoja, tutahakikisha kwamba mustakabali wa Kongo hauandikwi kwa damu ya vita, bali kwa matumaini, fursa, na ustawi.“
“Afrika Lazima Ichukue Hatua. Afrika Lazima Iongoze. Afrika Lazima Iponye.” Ameeleza