Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema
Serikali zote mbili zinatambua mchango mkubwa unaotokana na
wanataaluma ya Ukutubi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo
kwa Taasisi za Serikali na Taasisi binafsi hapa nchini.
Ameyasema
hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Mwinyi wakati wa ufunguzi wa Kongamano na
Warsha inayoenda sambamba na Mkutano Mkuu wa 51 wa Chama cha Wakutubi
Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa
Ndege jijini Zanzibar.
Amesema kuwa kujifunza kupitia huduma za
maktaba za kidijitali itakuwa chachu ya kuwarahisishia wananchi kupata
taarifa na habari sahihi kwa wakati sambamba na kujiongezea uwezo wa
kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa mtu mmoja mmoja
na jamii kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais amesema ni wajibu
wa wakutubi na watoa huduma za Maktaba kuwekeza katika elimu na ubunifu
ili kubaini vyanzo mbali mbali vya taarifa na maarifa vilivyopo kwa
ajili ya kuboresha huduma za maktaba katika mfumo wa kidijitali.
Makamu
wa pili wa rais wa zanzibar amesema Serikali inaendelea na azma yake ya
kujenga Mktaba kuu ya kisasa katika eneo la Maisara ambayo itakidhi
viwango vya kitaifa na Kimataifa ikiwemo huduma za kidijitali pamoja na
kujenga Maktaba kwa kila Wilaya ambazo zitafungamana na utoaji wa
huduma za kisasa kwa jamii husika.
Sambamba na hayo Makmu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar amewataka wakutubi kusimamia malengo ya Chama chao
kwa kuwaunganisha wanataaluma ya ukutubi katika kukuza ushirikiano wa
Taasisi wanachama katika utoaji wa huduma za maktaba na kuboresha
viwango vya huduma hio kwa Tanzania nzima.
Mhe. Hemed amesema
anatambua kuwa Sera ya Taifa ya Maktaba ipo katika hatua za mwisho hivyo
amewaagiza Wakuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMAZA)
kushirikiana na vyama wa wakutubi katika kuandaa miongozo mbali mbali
ambayo itarahisisha utekelezaji wa Sera hiyo na kuleta mabadiliko chanya
kwa tasnia ukutubi, huduma za maktaba na wakutubi wenyewe.
Nae
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis
Abdulla Said amesema kongamano hilo na warsha kwa wana taaluma ya
Ukutubi litaleta mabadiliko makubwa hasa katika upatikanaji wa taarifa
za usahihi, na zenye ufanisi na kuwafikia walengwa kwa wakati.
Khamis
amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar
imetenga bajeti maalum kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vyote muhimu vya
kusomea na kufundishia kwa ajili ya kuboresha huduma za maktaba ili
kuweza kuakisi mahitaji ya watumiaji.
Amesema Wizara ya Elimu
imejipanga kuimarisha Mifumo ya kidijitali katika Maktaba zote za
Zanzibar ambao utawezesha kuongeza ufanisi wa huduma za maktaba na
kupunguza changamoto ya upotevu wa vitabu pamoja na kuwapatia fursa za
mafunzo ndani na nje ya nchi wanataaluma ya ukutubi ili kuendana na
mabadiliko ya Teknolojia na ongezeko la mahitaji ya huduma za Maktaba
nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba
Tanzania Profesa Ali Mcharazo amesema wakati umefika kwa Wakutubi
kuwezeshwa kielimu na kupatiwa vifaa vya kisasa ili kuweza kufanya kazi
zao kwa uweledi na ubora wa hali ya juu katika kutoa huduma za Maktaba
nchini.
Profesa Mcharazo amesema wakutubi wana wajibu wa
kujiendeleza kitaaluma na kujifunza ubunifu katika kada yao kwa
kuzingatia kuwa Elimu bora hutegemea vifaa bora na wataalamu bora wa
kuisambaza elimu hio.
Mapema Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za
Maktaba Zanzibar Dkt. Ulfat Abdulaziz Ibrahim amesema Bodi ya Huduma za
Maktaba Zanzibar imejipanga kufanya Mapinduzi ya Kifikra juu ya maana,
matumizi na umuhimu wa Maktaba na wakutubi katika kufikia malengo ya
elimu Tanzania.
Dkt. Ulfat amesema kufanyika kwa Kongamano na
Warsha kwa Wakutubi wa Tanzania litasaidia kuongeza ujuzi na taaluma kwa
watatoa huduma hio kuweza kutoa taaluma bora kwa watumiaji wa Maktaba
popote walipo nchini.
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipokea
maelezo kutoka kwa Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Maktaba kutoka Bodi ya
Huduma za Maktaba Zanzibar Ndugu Ramadhan Said Yussuf wakati akikagua
kazi mbali mbali zinazofanywa na Wakutubi Tanzania kwa niaba ya Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussen Mwinyi
katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.