Serikali za
Tanzania na Algeria zimekubaliana kukuza diplomasia ya uchumi kwa
kutumia fursa muhimu za kiuchumi zinazopatikana katika nchi hizo mbili
ili kujenga ustawi wa watu wake.
Hayo yamejiri wakati Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo
(Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora
wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la
Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari,
2025 Addis Ababa, Ethiopia.
Viongozi hao wamejadili juu ya
umuhimu wa maandalizi ya Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ambapo mara ya mwisho
mkutano huo ulifanyika mwaka 2023 jijini Algiers, Algeria. Mkutano ujao
ulikubaliwa kufanyika mwaka 2025 nchini Tanzania hivyo, wamekubaliana
kuitisha mkutano mwingine mapema ili kuendana na makubaliano ya
kuanzishwa kwa tume hiyo yanaoelekeza kuitishwa kwa mkutano huo kila
baada ya miaka miwili ili kuruhusu ufuatiliaji wa utekelezaji katika
maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa.
Pia wamejadili kuimarisha
ushirikiano katika sekta ya elimu ambapo, Mhe. Attaf ameahidi kuwa
Algeria itaendelea kutoa fursa za ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na
mfupi kwa lengo la kujenga uwezo na uzoefu katika masuala mbalimbali ya
kitaaluma na kitaalamu.
Vilevile wamesisitiza umuhimu wa kukuza
ushirikiano katika sekta ya biashara, nishati na kwenye masuala ya
ulinzi, usalama. Pia, uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea
itakayotosheleza mahitaji halisi ya wakulima nchini Tanzania na
kuwezesha kuyafikia malengo ya Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ya
kuongeza ajira kwa vijana na kufanya kilimo biashara.
Ushirikiano
katika majukwaa ya kikanda na kimataifa ni miongoni mwa masuala
yaliyopewa msisitizo ili kuhakikisha nchi hizo mbili zinasimama imara
katika kuunga mkono masuala ya kimkakati na yenye maslahi kwa pande zote
katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf pembezoni mwa Kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kilichofanyika tarehe 12 na 13 Februari, 2025 Addis Ababa, Ethiopia.