Na.Elisa Shunda, Simanjiro, Manyara
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndugu Ally Hapi (MNEC), amewahakikishia wananchi, hususan jamii ya wafugaji na wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, kuwa chama hicho kitaendelea kuisimamia serikali ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinafanyiwa kazi kwa haraka na kwa ufanisi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Narakawo, kata ya Loibosireti wilayani humo, Hapi alisema kuwa CCM imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa serikali inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hasa katika kulinda masilahi ya wakulima na wafugaji.
“Chama cha Mapinduzi kipo bega kwa bega na serikali kuhakikisha kuwa wakulima na wafugaji wanafanya shughuli zao kwa amani na usalama. Tunatambua changamoto zilizopo, na tutaendelea kuisimamia serikali ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alisema Hapi.
Katika hotuba yake, Hapi alisisitiza pia umuhimu wa amani na usalama kwa maendeleo ya taifa, akieleza kuwa bila amani hakuna jambo lolote linaloweza kufanikiwa.
“Amani ni tunu kubwa kwa taifa letu. Bila amani, hakuna kilimo, hakuna ufugaji, hakuna biashara, na hakuna maendeleo. Hivyo, ni jukumu letu sote kulinda amani kwa kila hali,” aliongeza Hapi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Ndugu Ole Sendeka, alieleza namna serikali ya Awamu ya Sita inavyoshughulikia changamoto za wananchi kwa vitendo. Alibainisha kuwa moja ya hatua kubwa zilizochukuliwa ni ujenzi wa bwawa maalum kwa ajili ya mifugo, linalofadhiliwa na serikali, ili kusaidia upatikanaji wa maji kwa wafugaji.
“Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza ahadi zake kwa vitendo. Hili bwawa kwa ajili ya mifugo ni moja ya miradi muhimu iliyofanikishwa kwa fedha za serikali ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji kwa wafugaji wetu,” alisema Ole Sendeka.
Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Manyara naye alieleza jinsi serikali inavyofanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo ya kweli.
“Tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, tumeona mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali. Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ajili ya wananchi, na sisi kama viongozi tunaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na miradi hiyo,” alisema.
Viongozi wengine waliokuwepo, akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Manyara Janes Garabe na diwani wa kata hiyo Ezekiel Lesenga walizungumzia jinsi mipango ya serikali inavyowanufaisha wananchi na kutoa ushuhuda wa mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi walioshiriki mkutano huo akiwemo Lowasa Sindilopa na Daniel Pakasi walieleza kuwa licha ya kuwa na imani na serikali, bado wanahitaji hatua zaidi za kutatua changamoto zao, hususani zinazohusiana na upatikanaji wa marishsho ya mifugo na huduma bora za kijamii na miundombinu.
“Tuna imani na serikali, lakini bado tunahitaji msaada zaidi katika kutatua changamoto zetu. Masuala ya maji, barabara na huduma za afya yanapaswa kupewa kipaumbele zaidi,” alisema mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo.