Shirika la Water aid la nchini Uingereza linatarajia kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa uboreshaji miundombinu ya maji, vyoo bora na usafi wa mazingira utakaonufaisha wakazi 368,000 wa vijiji 96 katika kata 33 za wilaya ya Hanang mkoani Manyara kupata maji kwa asilimia 100 na kuondokana na changamoto ya magonjwa ambukizi yanayotokana na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji.
Akizungumza katika kikao cha kushirikisha wadau mjini Katesh wilayani Hanang, mkuu wa miradi wa WaterAid Tanzania Beda Levira amesema mradi huo unaotarajiwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu kwa sasa upo katika hatua za utafiti wa kujua mahitaji halisi ya wilaya ya Hanang na namna watakavyotekeleza mradi wakishirikiana na Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA.
Kwa upande wake mhandisi wa maji kutoka RUWASA Barnabas Taligunga amesema mradi huo utaongeza nguvu ya uboreshaji wa usafi wa miundombinu ya kusambaza maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwa watumiaji ili kudhibiti uwezekano kusambaa magonjwa kipitia maji.
Akizungumza kwa niaba ya katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, mganga mkuu wa mkoa wa Manyara Dkt ENDREW METHOD ametoa wito kwa viongozi wa halmashauri ya Hanang kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Water Aid kutekeleza mradi huo ili uwe mfano kwa wilaya zingine, huku mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Hanang Rose Kamili Sukum akishukuru shirika hilo kuchagua Hanang.
Mradi huu utakapokamilika, Hanang itatumika kama mfano kwa wilaya zingine kujifunza.
The post Mradi Mkubwa wa Maji na Usafi wa Mazingira Kuwanufaisha Wakazi wa Hanang first appeared on Millard Ayo.