NA BELINDA JOSEPH, RUVUMA
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeendelea na ziara yake ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme, Ziara hiyo imekita kambi eneo la Mitendewawa, kata ya Mshangano, ambapo wananchi wamejifunza hatua mbalimbali za kuhakikisha wanapata na kutumia umeme kwa usahihi.
Afisa Uhusiano na huduma kwa wateja TANESCO Mkoa wa Ruvuma Allan Njiro, ameeleza kwamba mradi mkubwa wa umeme umefanikiwa kutekelezwa Mitendewawa licha ya changamoto za upatikanaji wa vifaa maalum ambazo zilisababisha ucheleweshaji wa utekelezaji lakini kwa sasa jitihada zimezaa matunda.
Njiro amewashukuru wananchi wa Mitendewawa kwa uvumilivu wao wakati wa utekelezaji wa mradi huo huku akiwahakikishia kwamba tayari zimefungwa transfoma mbili kwa matumizi ya wananchi na mpango uliopo ni kuendelea na mradi mwingine ambao unatarajiwa kuanza ifikapo mwezi Julai, Aidha amekumbusha wananchi umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme ili kuepuka hasara kubwa na kuonya dhidi ya ukataji miti kiholela karibu na nyaya za umeme.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja msaidizi TANESCO Ruvuma, Emma Ulendo, amewashauri wananchi kufanya wiring kwa kutumia vifaa bora, huku akisisitiza kwamba maombi ya kuunganishiwa umeme yanaweza kufanywa kupitia ofisi za TANESCO au njia ya simu janja, au simu kitochi ambapo amewahimiza ulipaji wa gharama za kuunganishiwa umeme zifanyike kwa njia salama ili kuepuka udanganyifu na wananchi wanapaswa kutuma maombi haraka ili kufanikisha upatikanaji wa huduma ya umeme.
Diwani wa Kata ya Mshangano, Samweli Mbano, ameishukuru TANESCO kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya umeme, akisema kwamba itawasaidia wananchi kutumia umeme kwa usalama na kutunza miundombinu, aidha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme, akiongeza kuwa hatua hii ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na uchumi wa taifa.
Mbano amesisitiza kwamba upatikanaji wa umeme unaleta faida kubwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya ardhi na kusaidia katika shughuli za biashara na maendeleo kiuchumi, Elimu ya matumizi sahihi ya umeme itawawezesha wananchi kuepuka hatari za uharibifu wa miundombinu ambao unaweza kusababisha hasara kubwa kwa serikali na kuchelewesha huduma kwa wananchi.