
Dar es Salaam.
AIRTEL Tanzania imewasii wateja wake kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya utapeli wa fedha kwa njia ya simu, tatizo ambalo limekuwa likishika kasi kupitia jumbe na simu za udanganyifu.
Matapeli wamekuwa wakituma ujumbe kupitia namba zisizojulikana wakiwataka wateja watume pesa kama michango kwa ajili kupata uponyaji wa kiroho. Kufuatia matukio haya, Airtel Tanzania inawakumbusha wateja wetu wasitume fedha kwenda kwenye namba wasizozifahamu bila ya kuhakikisha mpokeaji wa fedha hizo.
Akizungumza kutokea makao makuu ya Airtel Tanzania, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano alisisitiza kuwa namba maalum ya mawasiliano kutoka kampuni ya Airtel ni 100.
“Wateja wanapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya utapeli wa simu au jumbe fupi zinazotoka kwenye namba za watu wanaodai kuwa ni wawakilishi wa Airtel Tanzania. Airtel inawasiliana na wateja wake kupitia namba 100 tu. Hakuna namba nyingine yoyote ambayo inatumika kuwasiliana na wateja wetu,” Alieleza.
Aliongea kuwa, “Watanzania wengi wamekuwa wahanga wa utapeli wa simu kwa kupokea jumbe kutoka kwenye namba mpya zinazowataka watume fedha. Hii ni kwasababu wanapopokea jumbe hizo wanadhani kuwa wanawasiliana na mtu wanaemfahamu. Tunawaasa wateja wetu kuhakiki na kujiridhisha kabla ya kufanya muamala wowote.”
Aidha, Singano aliwashauri wateja kulinda namba zao za siri na kutomwambia mtu yoyote hata kama wanawaamini. Alisema kuwa matapeli hutumia vibaya taarifa za watumiaji kupata akaunti zao na kufanya miamala isiyoidhinishwa.
“Nywila ni namba ya siri ya mtumiaji ambayo haitakiwi kutumiwa na mtu mwingine. Kumpa mtu mwingine hata yule wa karibu yako inaongeza hatari ya kuweza kutumika kwenye uhalifu,” alisisitiza..
Singano alibainisha kwamba Airtel Tanzania inaendelea kujidhatiti kulinda wateja wake na inawahamasisha watu wote kuwa makini na taarifa na kuripoti shughuli zozote zenye kutia mashaka ili waweze kulinda akaunti zao za simu.
“Simu ya mteja inapoibiwa, tunashauri wafanye yafuatayo haraka; toa taarifa polisi na uripoti namba zinazokupa mashaka kwenda namba 15040. Wateja wanapaswa kuhakiki namba zao zilizosajiliwa kwa kutumia namba ya kitambulisho cha NIDA kwa kupiga *106# ili kujihakikishia usalama. Hii inasaidia kutambua namba ambazo hazijaidhinishwa ambazo zimeunganishwa na kitambulisho chako kiholela. Kufanya hivyo kunazuia uwezekano kwa kutumika kwenye utapeli,” alisema.