Na. Najjat Omar
AZIMIO la Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu (UDHR) la mwaka 1948 ndiyo msingi mkuu wa maazimioyoteya haki za binadamu yaliyoridhiwa na mataifa mbalimbali duniani. Azimio hilo linazitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa ahadi ya kulinda haki na uhuru wa binadamu ambapo kifungu Na. 19 kinatamka kuwa; “Kila mtu ana haki ya uhuru wa maoni na kujieleza; hii haki ni pamoja na uhuru kutoa maoni bila kuingiliwa na kutafuta, kupokea na kutoa habari na mawazo kupitia vyombo vya habari vyovyote na bila kujali mipaka.”
Azimio hilo Tanzania imeliridhia na kwa upande wa Zanzibar suala la haki za binadamu liliingizwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka1984. Kifungu cha 18(1) … kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta kupokea na kutoa habari na mawazo kupitia chombo chochote, bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”
Pamoja na ahadi na dhima hiyo iliyochukuliwa na Katiba, uhuru ulioelezwa hapo umewekewa vigingi vingi kwa kutungwa sheria za kuudhibiti, hasa uhuru wa kutoa maoni, kukusanya, kusambaza na kujieleza bila kujali mipaka.
Sheria mojawapo yenye vikwazo kwa uhuru huo ni sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria No.8 ya 1997.
Kuna vifungu kadhaa ambavyo vimetajwa kwenye sheria hii vinayotoa mamlaka makubwa kwa viongozi wa serikali kudhibiti maudhui ya habari, huku ikikosa vifungu vinavyolinda uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa waandishi wa habari.
Kwa mfano kifungu cha 27(1), kinachoruhusu afisa wa polisi kukamata gazeti lolote linaloshukiwa limechapishwa kinyume na sheria, na Kifungu cha 31, kinachomruhusu Waziri kuzuia uchapishaji wa gazeti, vinaonyesha mamlaka makubwa waliyopewa baadhi ya watu na kuuweka uhuru wa habari mashakani.
Kwa zaidi ya miongo miwili sasa wadau wa habari wamekuwa wakichechemua kutaka sheria hiyo na nyingine kandamizi zinazokwaza uhuru wa habari zibadilishwe na jitihada zimefanywa hadi rasimu ya muswada wa sheria ya huduma za habari ikapatikana lakini kwa bahati mbaya muswada huo umekuwa ukipigwa danadana inashindikana kufikishwa Baraza la Wawakilishi ili ujadiliwe na hatimaye kutungwa sheria.
Sheria hiyo na nyingine nyingi zilizotungwa baada ya hiyo zimeathiri uhuru wa habari kwa kiasi kikubwa na wadau wamekuwa wakizipigia kelele toka mwaka 2008 lakini hadi leo kelele hizo hazijaganda masikioni mwa wenye mamlaka wanaoamua kipi kipelekwe Baraza la Wawakilishi na kipi kisipelekwe.
Zipo nchi ndani ya Afrika Mashariki ambazo zimepiga hatua katika kuhakikisha kuwa uhuru wa kujieleza, kutoa maoni, kupata taarifa na kusambaza unazingatiwa na sheria. Miongoni mwa nchi hizo ni Kenya na Rwanda…
Kenya imepiga hatua kubwa katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari, hasa baada ya kupitishwa kwa Katiba ya 2010. Ibara ya 34 ya Katiba inaweka ulinzi wa vyombo vya habari visiingiliwe na serikali. Wakati huo huo Sheria ya Baraza la Habari ya 2013 inasimamia vyombo vya habari kwa kuhakikisha uwajibikaji wa kitaaluma.
Nchi ya Rwanda imefanikiwa kuimarisha mazingira ya vyombo vya habari kupitia Sheria ya Vyombo vya Habari ya 2013. Sheria hii imeweka msingi wa uwazi na uhuru wa kupata taarifa kupitia sheria ya Haki ya Kupata Taarifa (2013). Ingawa bado kuna changamoto za kudhibiti maudhui na ufuatiliaji wa serikali, Rwanda inaonekana kuwa mfano wa maendeleo ya kidemokrasia katika sekta ya habari kwa kuweka ulinzi na uhuru wa upatikanaji wa taarifa.
Hali ikiwa hivyo katika nchi hizo, Zanzibar iko kwenye miongo miwili ya kulilia na kuitaka serikali kubadilisha baadhi ya vifungu kandamizi vya Sheria. Wadau wa habari Zanzibar wamekuwa wakipambana kutaka mabadiliko ya sheria hii ili iendane na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu kama Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – TAMWA –Znz, Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Klabu za Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wamekuwa mstari wa mbele kushawishi mabadiliko haya.
Wanaharakati wa haki za binadamu na wanahabari wamekuwa wakiibua mijadala kuhusu umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na hata uhuru wa kujieleza kwa maendeleo ya jamii, nchi na taifa husika lakini bado kelele hizo zimekuwa zikipita kwenye masikio yaliyowekwa nta.
Hata hivyo, mapambano haya yamefanikiwa kuongeza uelewa wa wadau, waandishi na hata wananchi juu ya umuhimu wa uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza lakini bado jitihada zao za kutaka kuiona Zanzibar ikiwa huru katika nyanja hiyo ambayo kimsingi ndiyo mhimili wa demokrasia, zimegonga mwamba kutokana na urasimu na ukosefu wa nia ya kisiasa.
Vyombo vya habari vingi Zanzibar vinahofia kuchapisha/kutangaza habari zinazoikosoa Serikali, kutokana na hofu ya kufutiwa leseni au kushitakiwa chini ya sheria hii na nyinginezo zilizopitwa na wakati. Kutokuwapo kwa sheria nzuri ya habari Zanzibar si tu kwamba kunadhoofisha vyombo vya habari, bali pia kunazuia maendeleo na ukuaji wa demokrasia.
Kimsingi vyombo vya habari ndiyo tegemeo kubwa la wananchi katikakupaza sautizawasio na sauti, kufichua ufisadi, na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi. Sheria iliyopo inahatarisha uwezo wa vyombo vya habari na wanahabari katika kufanikisha jukumu hilo.
Kwa Serikali sikivu tayari ingeyachakata maoni ya wadau wa habari na kuyafanyia kazi kwa kupitisha sheria mpya zinazozingatia viwango vya kimataifa vya haki na uhuru wa kupata, kukusanya, kusambaza taarifa na uhuru wa kutoa maoni.
Pamoja na juhudi za miongo miwili za wadau kupigania mabadiliko, bado kuna kazi kubwa ya kufanikisha mfumo wa sheria unaoendana na wakati wa sasa. Ikiwa serikali itakuwa tayari kushirikiana na wadau na kujifunza kutoka nchi jirani, Zanzibar pia inaweza kuwa mfano wa mageuzi ya sheria za habari Afrika Mashariki.