Na LG, Michuzi TV
MKURUGENZI Mtendaji Wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na mtaalam wa afya nchini Tanzania, Profesa. Mohamed Yakub Janabi ametangazwa rasmi kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Kanda ya Afrika.
Prof. Janabi anawania nafasi hiyo ili kuziba nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mteule wa Kanda hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile, Waziri wa zamani wa Afya wa Tanzania na mwakilishi kiti cha ubunge kupitia jimbo la Kigamboni aliyefariki Novemba 2024.
Kupitia tovuti ya Shirika la Afya Duniani Ukanda wa Afrika yamechapishwa majina ya watakaowania nafasi hiyo pamoja na wasifu zao (CV) ambapo Prof. Janabi anaongoza kwa CV yenye kurasa kumi iliyobeba uzoefu na ubobevu katika masuala ya afya.
Prof. Janabi ni miongoni mwa wagombea watano, ambao majina yao yataingia katika mchakato wa uchaguzi Mei 18, mwaka huu.
Aidha Prof. Janabi ni mgombea pekee kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, huku wagombea wanne wakiwakilisha nchi za Afrika Magharibi ambao ni Dk. N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast,) Dk. Dramé Mohammed Lamine (Guinea,) Dk. Boureima Hama Sambo (Niger,) na Pr. Mijiyawa Moustafa akiwakilisha Togo.