Na Mwandishi, Michuzi Tv
BANK OF AFRICA Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika huduma bora kwa wateja wake ili kuchochea maendeleo ya kifedha na ukuaji wa uchumi nchini.
Akizungumza kwenye hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Wasia Issa Mushi, alisema benki hiyo inapanua huduma zake kwa kuleta bidhaa mpya kama kadi za VISA na kadi za mkopo (credit cards).
“Tunataka kuwarahisishia wateja wetu upatikanaji wa huduma za kifedha kwa kuimarisha huduma zetu na kuja na bidhaa zinazokidhi mahitaji yao,” alisema Mushi.
Aliongeza kuwa benki hiyo inatilia mkazo uhusiano wa karibu na wateja wake wa viwango vyote—wakubwa, wa kati, na wadogo—ili kuhakikisha ustawi wa sekta ya kifedha na uchumi kwa ujumla.
Kwa sasa, BANK OF AFRICA Tanzania ina zaidi ya mawakala 200 nchini na inalenga kuongeza idadi hiyo hadi kufikia mawakala 500 mwishoni mwa mwaka huu. “Tunapanua mtandao wa huduma zetu ili kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa urahisi zaidi, hususan wafanyabiashara,” aliongeza Mushi.
Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Katibu wa Baraza la Ulamaa nchini, Shekhe Hassan Chizenge, aliipongeza benki hiyo kwa hatua yake ya kuandaa futari ya pamoja na wateja wake, akisema ni njia nzuri ya kuimarisha mahusiano.
“Ni jambo la heri kuona taasisi ya kifedha kama BANK OF AFRICA ikiweka mkazo katika kujenga mahusiano ya karibu na wateja wake kupitia hafla kama hii,” alisema Shekhe Chizenge.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Biashara wa benki hiyo, Hamza Cherkaoui, alisema benki hiyo itaendelea kuwekeza katika mifumo ya kidigitali na uvumbuzi wa kiteknolojia ili kuimarisha huduma zake.
BANK OF AFRICA Tanzania ilianza shughuli zake nchini mwaka 2007 baada ya kununua Benki ya Eurafrican, ambayo ilianzishwa Tanzania mwaka 1995. Benki hii ni sehemu ya BANK OF AFRICA GROUP, mtandao wa benki unaofanya kazi katika nchi 18 barani Afrika na pia kuwa na uwakilishi katika nchi kama Ufaransa, Hispania, Uingereza, na China.
Tangu mwaka 2010, benki hiyo imekuwa sehemu ya BMCE Bank ya Morocco, ambayo ni moja ya benki kubwa zaidi barani Afrika, ikiwa na matawi katika zaidi ya nchi 31.
Kwa sasa, BANK OF AFRICA Tanzania ina mtandao wa matawi 18, yakiwemo 9 Dar es Salaam na mengine mikoani kama Arusha, Mwanza, na Zanzibar, ikiwa na lengo la kufikisha huduma bora kwa wateja wake kote nchini.
