Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam imetia saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe kwa kiwango cha lami, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutatua changamoto ya foleni katika eneo hilo.
Hafla ya utiaji saini imefanyika leo Jumanne Machi 19, 2025 katika ofisi za TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo Meneja wa TANROADS mkoani humo, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema mradi huo utaanza mara moja baada ya kusainiwa kwa mkataba.
“Leo tumetia saini mkataba wa ujenzi wa njia nne kwa kiwango cha lami kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe, wenye urefu wa kilometa 3.8. Ujenzi huu utagharimu shilingi bilioni 54 na utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 kuanzia leo,” alisema Mhandisi Kyamba.
Mradi huo utatekelezwa na mkandarasi kutoka nchini China, STECOL Corporation, ambaye ameahidi kukamilisha kazi kwa ubora na kwa muda uliopangwa.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, Bw. Ma Ziheng alisema,
“Tutahakikisha tunazingatia viwango vya ubora na kukamilisha kazi kwa wakati kama mkataba unavyoelekeza.”
Barabara hiyo ni sehemu muhimu ya miundombinu ya jiji la Dar es Salaam, ambapo kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakikumbwa na foleni kubwa kuanzia Mbagala hadi Kongowe.
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutapunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo na kuinua kiwango cha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, kuwezesha maendeleo na kurahisisha maisha ya wananchi.
Itakumbukwa katika moja ya ziara zake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo la kutatua changamoto ya foleni katika eneo la Mbagala Rangi Tatu na maeneo mengine yenye msongamano mkubwa wa magari jijini Dar es Salaam.
Agizo hilo lililenga kuhakikisha kuwa serikali inatekeleza miradi ya miundombinu kwa haraka ili kuboresha hali ya usafiri na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Mhandisi Kyamba ameongeza kuwa mradi huu ni moja ya hatua madhubuti za serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam, kama ilivyoelekezwa na Rais Samia.
“Tunatarajia baada ya ujenzi kukamilika, changamoto ya foleni kuanzia Mbagala Rangi Tatu itakuwa historia,” alihitimisha.