Na: Calvin Gwabara – Nyandira.
Wakulima wa Kata ya Nyandira
Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro wamewaomba watafiti wa Mradi wa AGRISPARK
unaotekelezwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA
kuwatafutia mbinu za kukabiliana na wadudu aina ya Nzi weupe (White flies)
ambao wanaathiri mazao yao na kusababisha upotevu wa zaidi ya asilimia 70 hadi
80.
![]() |
Picha hii kwa msaada wa :https://www.ugaoo.com/blogs |
Ombi hilo limetolewa na wakulima hao wakati wa Watafiti kutoka SUA waliokwenda kukutana na wakulima kutambua changamoto na mahitaji yao ya maarifa ambayo ili kuandaa machapisho kwa lugha ya Kiswahili ambayo yatawaongezea maarifa wakulima na hivyo kuwasaidia kuboresha kilimo chao na kuinua kipato cha kaya hizo zilizo kwenye eneo la mradi huo wa utafiti wa AGRISPARK.
![]() |
Mkulima Peregrin Adam akizungumza na Wanafunzi watafiti wa mradi wa AGRISPARK kuhusu athari za Nzi weupe kwenye mazao yao. |
Akizungumza na watafiti hao
Mkulima Peregrin Adam kwa niaba ya wakulima wenzake amesema kuwa wadudu hao
hivi sasa wamekuwa tishio kwa wakulima shambani na hakuna dawa ambayo kwa sasa
inaweza kuwaangamiza kwakuwa wamekuwa wengi na unapojaribu kupuliza dawa wanaruka
ikiisha wanarudi na kuendelea kushambulia mazao.
“Tumefurahi sana kuwaona watafiti
kutoka SUA kuja kututembelea na kujua changamoto zinazotukabili, Kusema ukweli
kwa sasa changamoto kubwa kwenye kata hii yote ni hawa wadudu weupe huku
tunawaita “Masister” kutokana na weupe wao, hakuna dawa tena inayoweza kuwaua
wadudu hawa na wamejaa mashambani wanashambulia zaidi zao la maharage ambalo
ndilo zao letu kubwa la biashara kwenye kata yetu” Alieleza bwana Peegrini.
Aliongeza” Kiukweli kwa sasa
kilimo kimekuwa kigumu sana maana wanashambulia karibu mazao yote ya mbogamboga
ambayo ndio tegemeo letu kwa kipato kwa wakulima wote kwenye kata hii, na
wanatupa hasara kati ya asilimia 70 hadi 80 ya mazao yanapotea kutokana na
mashambulizi yao”.
Nae Adam mkulima mwingine wa
Nyandira ameiomba SUA kupitia kwa watafiti wake kuwasaidia kupata ufumbuzi wa
tatizo hilo na ikiwezekana kufikisha kilio hicho kwa serikali na wizara ya
Kilimo kuwatafutia ufumbuzi wa wadudu hao ambao wanawapa umasikini wakulima
wengi kwa sasa.
“Mkiangalia kwa mazingira yetu
huku tunalima mbogamboga msimu wote na tunategemewa sana kwa kuzalisha maharage
hasa mabichi kwenda mikoa mbalimbali hasa Dar es salaam na Dodoma lakini kwa
sasa uzalishaji wetu umepungua mno kutokana na kuongezeka kwa wadudu hawa
hatari wasiosikia dawa” alisema bwana Adam.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu mwenza wa
mradi wa AGRISPARK Dkt. Nicholous
Mwalukasa amesema kuwa lengo la kuwatembelea wakulima hao ni kutaka
kujua changamoto wanazokabiliana nazo katika kilimo ili waweze kutumia uwepo wa
machapisho mbalimbali ya kisayansi yaliyopo kuandaa vitabu vidogo ambavyo vitakuwa
na mada mbalimbali ili kutoa elimu ya
namna ya kukabiliana na changamoto zao ili kuongeza uzalishaji.
“ Hivi sasa tupo kwenye hatua ya
tatu ya mradi ambapo tumekuja kupata maelezo na changamoto zenu ili twende
kuwatafutia ufumbuzi wake kupitia tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani kote
na kwa kutumia wataalamu wa SUA na taasisi zingine na baadae tutatayarisha kwa
lugha rahisi ambayo mtaweza kuelewa na kutumia elimu hiyo kutatua changamoto
hizi” Alieleza Dkt. Mwalukasa.
Aliongeza “Kwanza niwape pole kwa
changamoto mnayokutana nayo kwa wadudu hawa na sisi tumelichukua na tunakwenda
kuwatafutia majibu sahihi na ya namna ya kuwakabili wadudu hawa pamoja na
changamoto zingine mlizoziainisha, tutaziandaa katika nakala ngumu na nakala laini
na kuwaletea ili muweze kupata maarifa hivyo kuendelea kulima kilimo chenye
tija na kujikwamua kujipatia maendeleo kupitia kilimo cha mbogamboga
mnachokifanya zaidi katika eneo hili”.
Watafiti hao kutoka SUA kupitia
mradi wa AGRISPARK wapo kwenye zoezi la kutembelea kata zilizo ndani ya mradi
huo kwenye Wilaya ya Mvomero, Manispaa ya Morogoro pamoja na Halmashauri ya
Wilaya ya Morogoro vijijini kwaajili ya kukutana na wakulima na wafugaji
kutambua mahitaji yao ya maarifa yanayoweza kusaidia kuinua uzalishaji kupitia
kilimo na mifugo katika mnyororo mzima wa thamni wa mazao na mifugo yao.
Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kama maono
mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwaajili ya kuwawezesha
watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WAKULIMA HAO WAKIZUNGUMZA NA WATAFITI KUHUSU CHANGAMOTO ZAO KWENYE KATA YA NYANDIRA.