Taasisi ya University of Dar es Salaam Computing Center (UCC) imeandaa warsha ya siku tatu inayolenga kujadili na kujenga uwezo kuhusu masuala ya usalama wa mtandao (cyber security) kwa wataalamu wake wa ndani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UCC, Bi. Leticia Ndongole, alisema kuwa lengo kuu la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo watendaji wa UCC katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazotokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani.
“Tumekusanyika hapa kwa ajili ya kufanya warsha ya siku tatu kuhusu usalama wa mtandao. Sisi kama UCC ni taasisi mwanzilishi ya masuala ya teknolojia hapa Tanzania. Tumekuwa tukitengeneza mifumo mbalimbali ya kiteknolojia inayotumika ndani ya serikali, sekta binafsi na hata nje ya nchi,” alisema Bi. Ndongole.
Bi. Ndongole aliongeza kuwa UCC pia inajihusisha kwa kiwango kikubwa na kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalamu pamoja na usimamizi wa mifumo ya TEHAMA kwa wadau mbalimbali wa sekta ya teknolojia.
Alisisitiza kuwa mabadiliko ya teknolojia duniani yamekuwa ya kasi kubwa, akitaja maendeleo kama vile akili bandia (Artificial Intelligence), sarafu za kidijitali kama Bitcoin na masuala mengine yanayokuja kwa haraka, huku pia akionya juu ya ongezeko la uhalifu mtandaoni ambalo ni changamoto si kwa Tanzania pekee bali kwa dunia nzima.
“Kwa kuwa sisi ni wataalamu wa kutengeneza mifumo, tunajua changamoto zipo wapi. Ndiyo maana tumeona ni vyema kufanya capacity building kwa watumishi wote wa UCC. Kupitia warsha hii tutakuwa na timu ya wataalamu mahiri wa usalama mtandaoni, ambao kwa siku hizi tatu wataongeza maarifa ya namna ya kuboresha mifumo yetu,” alieleza.
Bi. Ndongole aliongeza kuwa baada ya mafunzo haya, UCC itaweza kuongeza ufanisi katika kutengeneza mifumo mipya na kuimarisha iliyopo kwa lengo la kukidhi mahitaji ya serikali, sekta binafsi na watumiaji wa mwisho.
“Tunategemea kuwa mchango wetu kama UCC utaendelea kuleta mabadiliko makubwa katika serikali yetu, lakini pia katika nchi nyingine za Afrika. Tanzania kwa sasa ni ya pili barani Afrika kwa kasi ya kupokea teknolojia mpya, jambo linalotupa nafasi ya kuwa kinara katika mapinduzi ya kidigitali,” alisisitiza.
Kwa upande wake, mtaalamu wa mifumo ya usalama mtandaoni, Bw. Yusuph Kileo, alieleza kuwa suala la uhalifu wa mtandao kwa sasa ni changamoto kubwa kwa mataifa mengi duniani, kwani wahalifu hutumia mbinu mpya kila siku.
“Mafunzo haya ni ya kuongeza uwezo kwa watumishi wa UCC ambao sio tu hutoa mafunzo, bali pia wanatengeneza mifumo kwa taasisi za serikali na binafsi. Warsha hii itawasaidia kujifunza mbinu za kutambua changamoto za usalama, kuzizuia, na kujenga mifumo salama zaidi kwa matumizi ya kila siku,” alisema Bw. Kileo.
Aidha, alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kubaki salama wakati wanapofanya kazi katika mazingira mbalimbali ya taasisi, hasa wale wanaoshughulika na mifumo ya TEHAMA.
Warsha hiyo ya siku tatu inatarajiwa kumalizika kwa washiriki kuwa na uelewa wa kina juu ya mikakati ya kisasa ya kukabiliana na uhalifu wa mtandao, na kupelekea maboresho ya moja kwa moja katika maeneo yao ya kazi.