Na Said Mwishehe,Michuzi TV -Mbarali
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Stephen ametoa maelekezo kwa Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuweka utaratibu mzuri wa kugawa sehemu ya ardhi kwa wananchi wa Mbarali wayatumie kwa shughuli za kilimo.
Miongoni mwa ardhi hiyo ni sehemu ya mashamba yaliyokuwa ya serikali lakini wamepewa wawekezaji na wameshindwa kuyaendeleza ambayo sasa wamekuwa wakiwakodisha wananchi wanyonge.
Maelekezo ya CCM yametokana na malalamiko ya wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ambao wamesema kwa sasa wanashindwa kufanya shughuli za kilimo kwa sababu ya kuondolewa na serikali kupisha hifadhi ya Mto Ruaha na hivyo kuwa na hali ngumu kiuchumi, wanaiomba serikali iwaruhusu walime.
Akizugumza na wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya akiwa katika ziara ya kikazi, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira amesema CCM ni chama kinachotetea haki za wanyonge na hakitaki kuona wakinyanyasika au kudhulumiwa.
“Nimewasikiliza wananchi wa Mbarali kuhusu huu mgogoro wa aridhi, tumesikia kilio chenu na kazi yetu kubwa CCM ni kushughulika na matatizo ya watu. Mmezungumza kuhusu GN 28 ambayo hii tayari imefutwa maana ilinung’unikiwa na watu wote wa Mbarali.
“Hatuwezi kubaki nayo lakini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake alishaiondoa GN 28 ambayo ilikuwa imechukua vijiji 32 na kuwa sehemu ya hifadhi ya Mto Ruaha, sasa kuna GN 754 ambayo hii imeondoa vijiji 28 katika hifadhi na kuvirejesha kwa wananchi na vijiji vitano ambavyo vimebaki hifadhini vinaendelea kufanyiwa kazi,” alisema.
Hata hivyo, aliwaeleza wananchi hao kuwa Mwenyezi Mungu aliwaweka Mbarali karibu na Mto Ruaha, hawakujiweka, lakini mto huo umebeba hatima ya maisha ya Watanzania wote.
“Mkiua Mto Ruaha mtaua Watanzania wengine. Mmezungumzia umeme uliopo lakini umeme huo unatokana na Mto Ruaha.
“Huko nyuma tulitembelea Ihefu kuangalia hali halisi, ilikuwa imekauka watu wa mifugo walifuata malisho, Mto Ruaha maji yalikauka. Hatuwezi kuweka masharti ya kuumiza wananchi, tunajua maumivu yaliyopo lakini tuache Ruaha bila hivyo tutakufa wote.
“Sasa mgogoro ule wa ardhi ambao umesemwa na wananchi tunaushughulikia. Kwanza lile eneo lililochukuliwa na hifadhi halafu limetolewa na GN 754 lina ukubwa wa ekari 185,000 tayari limerudishwa kwa nje ya hifadhi, lakini kulikuwa kuna watu wameishi, kuna wengine wamtoka walikotoka wamekwenda katika maeneo hayo,” alisema.
Akieleza zaidi amesema kwa hali hiyo aliwataka waziri wa ardhi na mkuu wa mkoa wa Mbeya kwenda maeneo hayo ili watu waliokuwepo awali wapewe maeneo hayo kwanza na wapewe kwa haki baada ya kufanya uchunguzi.
Alisisitiza wananchi wapewe maeneo yao walime na kuongeza kuwa, Tanzania ni tofauti na nchi nyingine ambako wameuza ardhi lakini hapa nchini hakuna utaratibu huo.
Pia, Wasira alisema serikali iliwapatia wawekezaji ikiwemo Kampuni ya Mbarali Estate na Kapunga, ambazo walikubaliana nao kwani yalikuwa mashamba ya serikali na walikubaliana wayalime lakini wanalima kidogo na mengine kuyakodisha kwa wananchi.
“Wawekezaji hao wanakodisha mashamba kwa wananchi wenye hali mbaya kiuchumi. Sasa tunasema dunia ya samaki mkubwa anakula wadogo ina uzuri wake lakini gharama yake ni kubwa. Nimezungumza na mwekezaji wa Kapunga ana shamba namba moja na shamba namba mbili.
“Tumekubaliana sehemu ya mashamba hayo yatagawiwa kwa wananchi yawe mali yao kwa shughuli za kilimo badala ya kuendelea kukodishwa na wawekezaji na kazi hiyo ya ugawaji itasamamiwa na Waziri wa Aridhi na Mkuu wa Mkoa. Waliokuwa wanakodi wapewe mashamba na kazi yetu CCM ni kuwapa majawabu ya matatizo haya.
Kuhusu upande wa Madibila, Wasira alisema haiko mbali na Ihefu hivyo wananchi wasiende Ihefu lakini wapate maeneo ya kulima.
Awali Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo akuzungumza katika mkutano huo, aliiomba serikali kuwafikiria wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwa idadi yao ni kubwa na eneo wanalolitumia kwa shughuli za kilimo ni dogo na uchumi wao unategemea kilimo.