NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Emmanuel Tutuba amewatoa hofu wananchi kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza kikamilifu jukumu lake la msingi la la kuandaa la kujenga mfumo imara wa kifedha unaochangia uchumi imara endelevu wa nchi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Soko la Dunia.
Ameyasema hayo Machi 20,2025 kwenye hafla ya Iftar iliyoandaliwa na taasisi hiyo na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo wa kidini.
Tutuba ameeleza kuwa benki hiyo itahakikisha Inaweka sera yake nzuri ya fedha ambayo itadhibiti mfumuko mkubwa wa bei ambapo utawasaidia wananchi kuwa nafuu katika gharama za maisha.
Aidha Tutuba amewaasa wananchi kujiepusha na shughuli za mikopo umiza pamoja na upatu kwa kuhakikisha wanapata huduma za kifedha kwa watoa huduma ambao wana leseni halali kutoka Benki kuu.
Amesema kuwa huduma hizo za kifedha ikiwemo mikopo pamoja na masuala ya upatu wananchi wanaweza kupata katika halmashauri kwani wamezikasimisha madaraka ambapo zimepewa leseni za vikoba sambamba na sehemu za ushirika ambapo zimepewa leseni ya SACCOS.
Aidha Gavana Tutuba ametoa rai kwa watoa huduma za kifedha nchini,kufuata masharti ya Leseni kwa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji na kuhakikisha haziwaumizi wananchi kwani wakienda kinyume watachukuliwa hatua za kisheria.
“Watoa huduma wahakikishe wanafuata masharti ya Leseni la sivyo Benki Kuu inaweza kuwafutia leseni na kuwachukulia hatua kali za kisheria” Gavana Tutuba amesema.
Kwa upande wake Mufti Mkuu wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zuber amewataka watanzania kuzuia na kuziba viashiria ambavyo vinaweza kusababisha kuharibika kwa amani ya nchi.
Shekhe Zuber amesema mwaka huu ni wa kwenda na kauli mbiu isemayo wajibika, jitambue acha mazoea kwa lengo la kuhakikisha amani ya nchi inatunzwa ambapo amefafanua kuwa Tanzania ni ya mfano katika amani katika ukanda wa Afrika Mashariki kwani ndio kimbilio la nchi za jirani.