Na Mwandishi wetu, Mirerani
CHAMA cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) kimepanga kuanza ziara ya kutembelea matawi yake saba kwa ajili ya kusikiliza kero, changamoto na mafanikio waliyonayo.
Mwenyekiti wa MAREMA Elisha Nelson Mnyawi ameyasema hayo kwenye kikao cha kamati tendaji ya MAREMA, kilichofanyika katika ofisi za makao makuu yake yaliyopo mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro.
Mnyawi amesema MAREMA ndiyo msimamizi wa matawi yaliyopo maeneo ya Wilaya mbalimbali hivyo ni vyema kufanya ziara ya kutembelea na kuzungumza na wachimbaji kwenye matawi yao.
Amesema wameanza ziara yao kwenye Tawi la Mirerani kisha wataendelea katika matawi mengine ikiwemo Kiteto, Nadonjukini, Mbulu na Magugu/Magara.
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Tanzanite, Joseph Manga amesema viongozi hao watakapokuwa wanawatembelea wachimbaji kwenye matawi yao itakuwa jambo jema kwao.
Manga amesema wakifika kwenye matawi wataweza kutembelea machimbo na kukutana na wachimbaji wa madini ya dhahabu, Tomarini ya kijani, gaineti, chumvi na madini ya ujenzi.
Awali, MAREMA walitembelea Tawi la Mirerani na kusikiliza kero na changamoto zilizopo kwenye eneo hilo ambapo walikutana na kamati tendaji ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Peter Laizer na Katibu wake Rachel Njau.
Akizungumza kwenye kikao hicho Makamu Mwenyekiti Peter Laizer amesema hivi karibuni walikutana na Ofisa madini mkazi Mirerani George Kaseza na kuongea naye.
Laizer amesema miongoni mwa kero na changamoto walizowasilisha ni kibali kimoja cha kununua zana za milipuko kuuzwa Sh100,000 na ukitaka zana nyingine katika eneo lingine inatakiwa ulipe bei hiyo upya.
Amesema pia walifikisha suala la kutumika kwa chumba cha upekuzi wa wamiliki, mameneja na wenye leseni za kununua na kuuza madini, ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite ili kuondoa msongamano.
Mwenyekiti wa MAREMA Elisha Nelson Mnyawi amesema wao kama viongozi wanapaswa kukusanya matatizo ya wachimbaji na kuyafikisha Serikalini kwa njia ya mazungumzo.
“Sisi siyo wanaharakati ni viongozi wa wachimbaji hivyo tunapaswa kukutana na kukaa na Serikali na kutoa kero na changamoto zetu ili watatue kwa lengo la maendeleo ya sekta yetu ya madini,” amesema Mnyawi.