Na Said Mwishehe
MIAKA minne ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa madarakani tangu achukue uongozi wa Nchi imetimia Machi 19,2025.
Hakika tunajivunia kuwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, tunafurahia uongozi wake katika kipindi chote cha miaka minne…..Ndio tunaadhimisha miaka minne ya Rais Samia kiroho safi tu, Kwani kuna mtu anateseka?
Tunakumbuka Machi 19 mwaka 2021 Rais Samia aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Dk.John Magufuli, Ni pigo kubwa kuondokewa na Rais Magufuli lakini tunayo faraja ya kuwa na Mama Samia Suluhu Hassan.
Uongozi wa Rais Samia umetufuta machozi Watanzania; Unajua kwanini? Nchi imetulia, Nchi inasonga na maisha ya Watanzania yanaendelea.
Kauli mbiu yake ya ‘Kazi Iendelee’ imekuwa na tija kwetu,leo tunafurahia kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya, Mtangulizi wake alikuwa akisema ‘Hapa Kazi Tu’ na Mama Samia akasema ‘Kazi Iendelee.’

Miaka minne ya Rais Samia madarakani tumeshuhudia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miradi ya kimkakati.Hakika Rais Samia amedhihirisha kwa vitendo dhamira yake njema kwa Taifa hili.
Miradi yote mikubwa imetekelezwa tena kwa kasi,ninaposema kasi unielewe basi.Ndio kila mradi umetekelezwa kwa kasi na mingine bado inaendele kutekelezwa, Nenda bwawa la Mwalimu Nyerere tayari limekamilika kwa asilimia 100,umeme umeanza kuzalishwa na hatuna tena uhaba wa umeme.
Miaka minne ya Rais Samia tunashuhudia ujenzi wa reli ya mwendo kasi maarufu kama SGR unavyoendelea kuchanja mbuga,wakati anachukua uongozi wa Nchi ujenzi wa reli ya SGR ulikuwa umetoka Dar hadi Morogoro.
Hata hivyo haukuwa umekamilika lakini leo tunapoadhimisha miaka minne ya kuwa madarakani reli ya SGR imefika Makutupola mkoani Singida.Lakini tayari kuelekea Tabora,Mwanza na Kigoma nako ujenzi wa SGR umeanza kunoga.
Wasukuma,Wanyamwezi na Waha wa Kigoma jiandaeni kusafiri kwa SGR wala sio miaka mingi kuanzia sasa.Tuna Samia anajua umuhimu wa reli hiyo kwa watu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kwa Dar, Moro hadi Dodoma ni mwendo mtelezo tu,SGR iko kazini.Watu na vibegi vya matairi kama Ulaya vile ,ndani ya treni watu wanabugia vikorosho,kahawa na anayetaka vinywaji vipo.
Treni tuliyokuwa tunaiona kwenye picha za akina Jet Lee na mwenzake Check Norris leo tunayo Tanzania halafu hata Pugu Stesheni inasimama mimi huyo Majohe Kwanzoma.
Hahakika Rais amesimamia vema kauli mbiu yake ya ‘Kazi Iendelee,’ ukweli sote ni mashahidi kazi inaendelea na tunaona.
Rais Samia ni Mama, Ni Super Women wa Taifa la Tanzania,hakuna kilichosimama, kila mradi ambao uliachwa na mtangulizi wake umetekelezwa na wanaokwenda mikoa ya Tanga,Kilimanjaro na Arusha pale daraja la Mto Wami wanateleza ambapo wakati Rais Samia anachukua madaraka ujenzi ulikuwa chini ya asilimia 20 lakini leo hii mabasi yanapita katika daraja jipya. Watu hawana tena ile hofu waliyokuwa nayo miaka ya nyuma.
Daraja la Wami lilikuwa linatishia usalama wa abiria na watumiaji wengine wa daraja hilo.Chini ya Rais Samia leo mambo muswano.Huo ni mfano mdogo tu.
Wakati Rais anachukua nchi kuna baadhi yetu waliamini Mama hataweza ,Nchi haitakuwa salama lakini Rais Samia amethibitisha yeye ni Super Women,yeye ni Malkia wa Nguvu.
Ameshika Nchi na hakika tuko salama salmini kabisa….Ahsante Rais wetu kwa utulivu huu uliopo katika ardhi yetu nzuri ya Tanzania.
Wakati tunaadhimisha miaka minne ya Rais Samia tunakumbuka alivyokuja na zile R nne.Lakini ngoja niguse tu ile R ya maridhiano ambavyo imeleta faraja kwa wananchi lakini ilivyopeleka kicheko kwa wanasiasa.
Huko nyuma wanasiasa walipigwa pini hakuna cha mikutano ya hadhara wala mama yake mikutano.Wakawa wanalalamika tu pembeni maana walibanwa wakabanika.
Rais Samia alivyoingia madarakani akatoa ruhusa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa.Na sio mikutano tu hata wanaotaka kuandamana ruksa.
Ndio, Ni kipindi ambacho hata waliokuwa wanaandamana walipoishiwa nguvu polisi waliwasaidia .Hiyo tumeshuhudia kwa Rais Samia tu katika uongozi wake.
Awamu ya Tano wapinzani hawakuwa na ujanja walikuwa kimya,hakuna mkutano wala maandamano.Hawakuthubutu na wengine walikimbia Nchi.
Hivyo wakati tunaadhimisha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani tunasema ahsante kwa kuja na R nne kwani zimeleta utulivu .
Hata wale waliokuwa wamekimbia nchi leo tunao,wanatamba tu huko mtaani.Wameshasahau yaliyowatokea.Watu bwana kweli tumeumbwa wa kusahau.
Rais Samia nakupongeza kwa uongozi wako katika miaka minne yako ajira mpya za kumwaga,wakati unachukua nchi ajira mpya zilikuwa 7000 lakini katika muda wa miaka minne umetoa ajira mpya 34000 na mikakati ya kuajiri zaidi imeendelea kuchukuliwa.
Nenda katika sekta ya afya ,bajeti ya dawa na vifaa tiba imeongezwa,ujenzi wa miundombinu ya Zahanati,Vituo vya afya na Hospitali za Rufaa zimejengwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia.Hongera Mama Super Women ,Mama Samia Mitano tena!
Kuna mengi yamefanywa na Rais Samia katika kipindi cha miaka minne, makusanyo ya kodi yameongezeka na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) inajivunia.
Kwa mfano tu katika kipindi cha Januari 1 mwaka huu wa 2025 TRA imevunja rekodi ya makusanyo tangu kuanzishwa kwake kwa kukusanya Sh.Trilioni 3.587 kwa mwezi Desemba.
Hivyo ukisikia Watanzania wanasema wana imani kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kwasababu anayofanya yanaonekana. Amefanya na anaendelea kufanya kwa ajili ya kubadilisha maisha ya Watanzania kutoka haya ya sasa na kuwa bora.
Katika miaka minne ya Rais Samia ametufundisha kuwa nchi inaweza kusonga mbele bila ya kuumiza wengine,anaamini katika haki,anaamini katika kujenga Taifa linaloishi kwa misingi ya kuheshimiana.
Lakini ngoja nikwambie tu katika sekta ya michezo unakumbuka goli la Mama ambavyo limeleta hamasa katika michezo na hasa mchezo wa soka.
Miaka minne ya uongozi wake timu za Simba na Yanga zimevuna mamilioni ya fedha. Goli la Mama limeleta chachu katika mpira wetu.
Hata hivyo Rais Samia ameweka nguvu katika michezo yote na kote huko amekuwa akitoa fedha kama sehemu ya kuhamasisha michezo. Hapo sijagusia ujenzi wa miundombunu ya viwanja vya michezo mbalimbali.
Miaka minne ya Rais Samia inaacha alama ya mbegu nzuri aliyoipanda katika sekta ya michezo.Tunakupongeza Rais Samia, wadau wa michezo wanathamini na kuheshimu jitihada zako…
Pamoja na yote hayo nikiri Rais Samia anaongozwa na Utu,uwajibikaji,uwezo,uvumilivu,uzalendo na ushawishi.Hakika watanzania tunajivunia uongozi wa Rais Samia,upendo wake kwetu hauna hata chembe ya shaka.Rais Samia katika miaka minne ametuonesha upendo wa kweli.
Hata hivyo nihitimishe kwa kusema tu katika miaka minne ya uongozi wa Rais Samia bila kujali anapitia changamoto gani uso wake muda wote umejaa tabasamu,uso umejaa nuru inayoangaza maisha ya Watanzania.
Jicho lake sasa,linaona wema na wabaya lakini cha kufurahisha alishasema Ukizingua atakuzingua….Mama Samia Super Women,Mama Samia mitano tena.
Kwa haya ambayo Rais Samia ameyafanya katika miaka minne amejikuta amekuwa kipenzi cha Watanzania,wanamsubiria tu katika uchaguzi mkuu wampe kura halafu iwe Mitano Tena…
Watanzania wanasubiria tu tarehe ya Uchaguzi Mkuu itangazwe na wakati ukifika wachukue, waweke Waaa…habari ya No Reform No Election wanaona kama haiwahusu vile, Ni kauli ya blaza na ndugu zake.Imeisha hiyoooo ,ni MAMA SAMIA TU, Wengine mbwembwe tu.
Simu 0713833822/0762451570.