Said Mwishehe,Michuzi TV-Kagera
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema kuwa Chama kinafahamu changamoto ambazo vijana wanakumbana nazo na kwamba Ilani ijayo ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030, itakuja na majibu ya shida zao.
Wasira ameyasema hayo leo Machi 22, 2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kemondo Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
“CCM inajua matatizo ya vijana, na imekuwa na mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto za vijana. Kwanza CCM imenzishwa na vijana kwani Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na miaka 32.
“Lakini hakuna chama cha wazee peke yao labda kiwe chama cha wazee, lakini chama cha siasa lazima kiwe na vijna, kijue matatizo ya vijana na kutafuta ufumbuzi wake,” amesema Wasira.
Amefafanua katika kutatua changamoto za vijana CCM kupitia Ilani yake ijayo ya Uchaguzi Mkuu itakuja na majibu ya matatizo ya vijana kutafuta ufumbuzi wake na kusisitiza katika Ilani inayokuja imekubalika vijana ni lazima wapewe nafasi.
Wasira alisema katika maisha ya leo vijana hawataki kusubiri fedha zinazokuja baada ya miezi sita, “wanataka wafanye mradi leo na wapate fedha hapo hapo wanunue vocha kuona mambo yanayoendelea duniani.”
Wasira alisema CCM ni lazima itakuja na majibu ya vijana na kwamba tayari hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ikiwemo kubadilisha mfumo wa elimu kwa kuwa na ufundi stadi kwa kuanzisha vyuo vya ufundi kupitia VETA.
Akifafanua zaidi alisema kumekuwepo na changamoto ya ajira tatizo ambalo linatokana na maendeleo kwa kuwa zamani kulikuwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mhitimu alipomaliza chuo alipata kazi moja kwa moja kwani kulikuwa na kazi lakini wa kufanya kazi hizo hakuna.
“Wananchi waliomaliza chuo kikuu walikwenda kazini moja kwa moja maana walikuwa wanasubiriwa na hata waliokuwa wanamaliza elimu ya darasa la nane nao waliajiriwa.
“Kutokana na maendeleo yaliyopo nchini tunavyo vyuo vikuu 49 vikiwemo vya Serikali, binafsi pamoja na vinavyomilikiwa na mashirika ya dini. Hivyo wanaomaliza kila mwaka ni wengi. Mimi ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere…
“Huwa ninaona wahitimu ni wengi mpaka najiuliza watakwenda wapi. Sasa tumebadili mfumo wa elimu ndio maana tunakuja na VETA kila wilaya. Tunataka vijana wafundishwe masomo ya utalaamu na wakienda VETA wanakamilisha utalaamu.”