DENIS MLOWE, IRINGA
Baada ya kuhairishwa uzinduzi wa mashindano ya Kombe la Vunja bei Machi 19 sasa rasmi ku,zinduliwa Eid Pili (April 2) katika kiwanja cha Kalenga kilichoko wilaya ya Iringa vijijini mkoani hapa huku uzinduzi huo ukisindikizwa wasanii maarufu kutoka jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa ya uzinduzi huo msemaji wa kampuni ya Vunja Bei ,Said Malekela alisema kuwa mechi ya Ufunguzi itakuwa kati ya wenyeji Kalenga fc watapambana na Mgela fc ambapo shughuli za uzinduzi zitaanza saa nne asubuhi mpaka 12 jioni kwa kuambatana na matukio mbalimbali ya kiburudani.
Alisema kuwa baada ya kuhitimisha mzunguko wa kwanza ulioshirikisha timu zaidi 140 kwa njia ya mtoano na kupata timu SO, ili ziingie rasmi kwenye Ligi ya Vunjabei Cup 2025 kumtafuta bingwa atakae jinyakulia shilingi milioni kumi (10,000,000/=),.
“Sasa tunautangazia umma wa watanzania na wanamichezo kwa ujumla kuwa awamu ya kumpata bingwa huyo itaanza rasmi siku ya IDDY PILI mwezi Aprili, 2025. Uzinduzi wa michuano hii utafanyika kiwanja Cha mpira wa miguu cha Kalenga na kupambwa na burudani mbalimbali za wasanii A list” Alisema
Alisema kuwa umechaguliwa uwanja wa Kalenga kwa kuwa timu zote 50 zitapaswa kuwepo uwanjani, zikitokea kata mbalimbali za wilaya ya Iringa, kwani wamemeona kata hiyo inafikika kirahisi kwa kata zote mkoani Iringa.
Malekela aliongeza kuwa siku ya uzinduzi licha ya kuwa na mechi rasmi ya uzinduzi kutakuwa na mechi ya utangulizi kati ya timu ya IDFA vs timu ya FRAT RG.
Aliongeza timu zote 50 zinatakiwa kuwa katika viwanja hivyo kwani kutakuwa na matukio ya ugawaji wa vifaa vya michezo kwa timu zote 50 na wasimamizi, burudani mbalimbali zitakazoongozwa na wasanii mbalimbali kutoka Dar es salaam.
“Ratiba ya shughuli zote itaanza asubuhi saa 4 hadi saa 12 jioni mwezi huu wa Machi tumeutumia vizuri kukamilisha mahitaji yote ya michuano ikiwemo kuandaa vifaa, semina kwa timu zote na kuandaa zawadi” Alisema
Alikipongeza Chama cha Soka cha wilaya (IDFA) na kamati ya Mashindano ya Vunjabei Cup 2025 kwa kusimamia vizuri awamu ya kwanza ya Mashindano hayo na imani ya kampuni kuwa awamu ya pili itafanikiwa zaidi.
Kwa upande wake Katibu wa mashindano Pastor Kwambiana alisema kuwa mara baada ya mechi ya Uzinduzi ratiba ya mashindano hayo itaendelea April 3 kwa timu nne kuumana katika viwanja viwili tofauti ambapo timu ya Mseke fc wataumana vikali dhidi ya Sadan fc katika mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Tanangozi.
Mchezo wa pili katika siku hiyo utakuwa kati ya Magic Site dhidi ya Super Eagle ambao utafanyika katika kiwanja cha Kwakilosa
Ametoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye mashindano hayo yatakayoendelea siku zote hadi kuhitimishwa kwake na kumpata bingwa atayejinyakulia kitita cha milioni 10.