Na John Walter -Mbulu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Bi. Rehema Said Bwasi, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake kubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo, hususan katika sekta ya elimu.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Bi. Rehema amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Halmashauri ya Mji wa Mbulu imepokea shilingi bilioni 6.1 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule za msingi.
Fedha hizo zimetumika kujenga shule mpya ya Msingi Hailotho kwa shilingi milioni 348 katika Kata ya Nambis, pamoja na ujenzi wa mabweni ya watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Endagikot kwa shilingi milioni 180.
Mabweni hayo yamewasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, Mkurugenzi ameeleza kuwa Halmashauri imepokea shilingi bilioni 13.1, ambazo zimewezesha ujenzi wa shule mpya mbili za sekondari.
Shule ya Sekondari Isale, iliyopo katika Kata ya Imboru, imepokea shilingi milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nane, jengo la utawala, maabara tatu, matundu 19 ya vyoo, na jengo la kompyuta.
Aidha, ujenzi wa Shule ya Sekondari Gunyoda unaendelea kwa shilingi milioni 584.
Mkurugenzi amesisitiza kuwa uwekezaji huo umeleta mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano darasani, kupunguza mimba za wanafunzi wa kike, kupunguza umbali wanaotembea wanafunzi kwenda shuleni, na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, hali ambayo imepunguza utoro.
Hata hivyo, Bi. Rehema amebainisha kuwa changamoto kubwa inayokabili sekta ya elimu kwa sasa ni uhaba wa nyumba za walimu, hivyo akaomba serikali kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo kwa kuwa ni kilio cha walimu wengi katika halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Bi. Rehema ameendelea kuhimiza ushirikiano kati ya serikali, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa maendeleo hayo yanadumu na elimu inazidi kuboreshwa kwa ustawi wa taifa.
Kwa upande wake, Mwalimu Filemoni Nade wa Shule ya Sekondari Chief Sarwat, ambaye amesimamia ujenzi wa Shule ya Sekondari Isale, alisema kuwa kabla ya shule hiyo kujengwa, wanafunzi walilazimika kutembea umbali mrefu na hata kuvuka mto, hasa wakati wa msimu wa mvua, jambo lililosababisha baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa ujenzi wa shule hiyo umeongeza mwitikio wa wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza, hasa wanafunzi wa kike wakinufaika kwa kuwaepusha na changamoto na vishawishi vinavyotokana na kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.
Nao wanafunzi waliotoa maoni yao wamesema kuwa mazingira ya kusomea yameimarika, hali ambayo inawapa uhuru na utulivu wa kujifunza, huku wakishukuru serikali kwa kuwajali.