Na Albano Midelo
Idara hii, ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora.
Maono ya Rais na Jitihada za Idara
Afisa Mthibiti Ubora wa Shule wa Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma, Mwl. Rehema Haule, anasisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa mwanga mkubwa kwa sekta ya elimu na kwamba Kupitia maono yake, Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule inatekeleza mikakati madhubuti ili kuboresha elimu katika ngazi zote.
“Idara hii ni jicho la Wizara ya Elimu kwani ina jukumu la kusimamia, kufuatilia, na kuboresha viwango vya elimu nchini’’,anasema na kuongeza kuwa Kupitia juhudi hizo, serikali imeweza kufanikisha malengo mengi ya elimu bora, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Muundo wa Idara na Majukumu Yake
Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule inaongozwa na Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule, akisaidiana na Wakurugenzi Wasaidizi katika vitengo vya Elimu ya Msingi, Elimu ya Sekondari, Vyuo vya Ualimu, na Maendeleo ya Wananchi.
Kulingana na Haule,Katika ngazi ya Halmashauri, kuna Maafisa Uthibiti Ubora wa Shule wanaoshirikiana na wathibiti wengine ili kutimiza majukumu yao ya kila siku.
Mwl.Haule anabainisha kuwa Katika utekelezaji wa majukumu yake, Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule inatekeleza kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kufanya tathmini ya jumla ya shule kwa kutembelea na kujiridhisha kuhusu hali halisi ya shule na Kusimamia na kuinua viwango vya elimu katika shule za awali, msingi, sekondari, na vyuo vya ualimu.
Majukumu mengine anayataja kuwa ni Kufanya tathmini ya ufuatiliaji ili kuhakikisha maboresho yaliyopendekezwa yanatekelezwa,Kufanya tathmini maalumu kwa madhumuni mbalimbali kama usajili wa shule na kushughulikia changamoto zinazojitokeza na Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau wa elimu kila inapohitajika.
Kwa mujibu wa Afisa Uthibiti huyo,majukumu mengine ni Kuwajengea uwezo walimu katika kutekeleza majukumu yao, hususan mbinu bora za ufundishaji.Kuandaa ripoti za tathmini na kuzifikisha kwa wadau wa elimu kama vile Kamati za Shule, Maafisa Elimu wa Kata, na Wizara ya Elimu na Kufanya tafiti za kutatua changamoto katika sekta ya elimu.
Umuhimu wa Elimu Bora kwa Maendeleo ya Taifa
Maendeleo ya taifa lolote yanategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa elimu inayotolewa kwa wananchi wake. Elimu bora inawapa watu ujuzi na maarifa, hivyo kuwa msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) inaeleza kwa kina umuhimu wa uthibiti wa ubora wa elimu, jambo linalosisitizwa na Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule.
Kwa mujibu wa Idara hiyo, wadau wote wa elimu wanapaswa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vinaendelea kuimarika.
Ofisa Uthibiti huyo wa Ubora wa shule katika Wilaya ya Nyasa anawahimiza wadau wote wa elimu kuwasiliana na ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule kabla ya kuanzisha shule au kufanya maamuzi muhimu kuhusu elimu ili kupata ushauri wa kitaalamu.
Hata hivyo anasema Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule inaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa elimu inakuwa chachu ya maendeleo ya taifa. Kupitia maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu, Ubora wa elimu nchini unaendelea kuimarika.
Haule anawakaribisha wadau wote wa elimu, wakiwemo walimu, wazazi na wananchi kwa ujumla, kutembelea ofisi zao ili kupata ushauri wa kitaalamu na kusaidia kuleta mageuzi chanya katika sekta ya elimu Tanzania.
Afisa Uthibiti Ubora wa Shule katika Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma
Jengo la Ofisi ya Uthibiti Ubora wa Shule wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Shule mpya ya msingi katika Kata ya Kilosa mjini Mbambabay iliyojengwa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia program ya BOOST.Sekondari ya Kata ya Liwundi wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ambayo imejengwa na serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia program ya Uboreshaji Elimu ya Sekondari SEUIP.