Wananchi
wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga wamemshukuru Mbunge wao, January
Makamba, kwa juhudi zake za kutatua kero mbalimbali zinazowakabili, huku
wakieleza kwamba watamchagua tena wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika
Oktoba mwaka huu.
Wakizungumza wakati wa ziara ya Mbunge huyo ya
kusikiliza kero na kutoa majawabu aliyoifanya katika kila kijiji cha
jimbo hilo, wananchi wamesema jitihada anazozifanya Mbunge wao kutatua
changamoto katika sekta zote, wanasisitiza kuwa lazima wamchague tena.
“
Sisi wananchi wa Bumbuli hatuna deni na wewe kwa sababu umetufanyia
mengi, tena mengine kwa pesa zako za mfukoni. Hivyo, sisi tunaenda na
wewe na hatutokuacha. Jibu letu utalipata Oktoba kwenye sanduku la
kura,” alisema Christina Kupaza, mkazi wa Vuga.
Said Dhahabu,
mkazi wa kijiji cha Manga Funta, alieleza sababu za kumchagua tena
Mbunge huyo kutokana na namna alivyoisaidia jamii yao kutatua tatizo
kubwa la maji, ambalo awali lililazimu wananchi hao kutembea umbali wa
kilometa nne juu ya mlima ili kufuata maji.
” Ndoa zetu ziliyumba
kwa sababu wake zetu walikuwa wanatembea usiku kuchota maji. Lakini
baada ya Mbunge wetu kusikia kilio chetu, alituletea rola za maji, sasa
tunapata maji ya bomba majumbani mwetu, na wengine wanachota karibu na
nyumba zao,” alisema Said Dhahabu.
Mariam Mdoe alieleza kuwa
changamoto ya maji ilipelekea baadhi ya wasichana kukosa wachumba, kwani
wanaume wa mjini walikuwa wakidai hawezi kuwaoa wakati kwao hakuna
maji. Hata hivyo, sasa wanapata huduma hiyo kwa urahisi baada ya Mbunge
kuwapelekea maji.
Diwani wa Kata ya Funta, Francis Kanju,
alisisitiza kuwa kwa yale aliyoyafanya Mbunge huyo, bora yeye asipate
udiwani, lakini wamchague tena January Makamba ili aendelee kuwaongoza
kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Diwani wa Kata ya Vuga,
Jumaa Dhahabu, alifafanua kuwa Mbunge huyo ni kiongozi wa kipekee ambaye
anaweza kuwasaidia wananchi wake bila kusubiri serikali.
Aliongeza kuwa katika Kata ya Vuga, Mbunge amefanya mengi ikiwemo
kuwajenga shule, zahanati, na kutatua changamoto ya umeme ambapo kila
kijiji kimepata umeme, kasoro vitongoji vichache ambavyo tayari ameahidi
vitapata umeme. Aidha, aliendelea kusema kwamba miradi mikubwa ya maji
imeanzishwa, na wananchi wameshuhudia mabadiliko makubwa baada ya mbunge
huyo kuwaongoza
” Mbunge wetu, hata kama hutatokea siku ya
uchaguzi, leta shati tu, tutalichagua maana umefanya mengi ambayo
hayajawahi kufanywa na Mbunge mwingine aliyepita,” alieleza Diwani wa
Vuga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kudumu wa Kamati ya Elimu, Afya, na
Maji katika Halmashauri ya Bumbuli.
Wananchi wengine kutoka
Mgwashi na kata ya Kongoi walieleza kuwa hawana shaka ya kumchagua tena
Mbunge wao wakati wa uchaguzi mkuu ujao, kwa kuwa amewafanyia mengi
katika sekta zote muhimu. Hata hivyo, walieleza kuwa wanatarajia utatuzi
wa changamoto ndogo ndogo zinazohusiana na barabara.
Hassani
Kupaza kutoka kata ya Tamota alisisitiza kuwa Mbunge wao anastahili
kupata miaka mitano mingine ya uongozi, kwa sababu tangu dunia iumbwe,
kijiji chao hakikuwa na umeme wala huduma zingine. Lakini sasa huduma
hizi zinapatikana kwa urahisi, ingawa changamoto hazijaisha, wameweza
kutatua asilimia kubwa ya matatizo.
Kaimu Meneja wa Wakala wa
Mjai vijijini (RUWASA) wilaya ya Lushoto Seleman Mdoe amesema katika
Halmashauri ya Bumbuli jumla ya miradi Miwili ya maji yenye thaman ya
sh.3.9 billion inaendelea kutekelezwa nakwmaba itakapokamilika jumla
ya vijiji 10 vitanufaika.