– AWATAKA WATAZANIA KUMUOMBEA AFYA NJEMA AWEZE KUFANYA MAKUBWA ZAIDI
Na Seif Mangwangi, Arusha
ALIYEKUWA kamanda wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na kada maarufu wa chama hicho, Justine Nyari amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni kiongozi wa mfano dhidi ya Mataifa Duniani na kuwataka watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao kumuombea afya njema ili aendelee kufanya mambo mazuri.
Akizungumzia miaka minne ya utendaji wa Rais Dkt Samia, Nyari amesema Rais Samia ametumia miaka yake vizuri kuwaletea watanzania maendeleo makubwa kwa miaka michache aliyoongoza.
” Tumeona mageuzi na maboresho makubwa katika sekta za kilimo, afya, madini,utalii, umeme, maji, elimu, viwanda, mazingira na hata diplomasia ya kimataifa, amefanya mambo ambayo Dunia yenyewe inajiuliza Rais Mwanamke amewezaje kufanya mambo yote haya tena kwa miaka michache tu madarakani,”amesema.
Amesema katika utawala wake wa miaka minne Rais Samia ameweza kuboresha sekta ya elimu kwa kuongeza madarasa, nyumba za walimu, kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kubadili mfumo wa elimu ili watoto waweze kufundishwa masomo ya kuwawezesha kujitegemea na elimu bure kwa kila Mtanzania.
Nyari ambaye pia alishawahi kuwa diwani kata ya Mirerani na mwaka 2015 kugombea ubunge jimbo la Arusha mjini na kushika nafasi ya pili ndani ya mchakato wa CCM, amesema maboresho hayo katika sekta ya elimu ndio yaliyomvutia na yeye kuamua kuwekeza kwa kujenga shule ya msingi ya Glisten Pre & Primary School iliyoko Mirerani wilayani Simanjiro lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika sekta hiyo.
” Mama amekuwa akihamasisha uwekezaji, hasa kwa watanzania, binafsi kama mfanyabiashara na kada wa CCM niliamua kuunga mkono jitihada za Rais wetu nimejenga shule hapa Mirerani na imekuwa ikifanya vizuri sana, watoto wetu wanafaulu sana wanapangiwa hadi shule za vipaji maalum kama Ilboru, Tabora Girls, Msalato n.k” anasema.
Nyari ambaye pia ni mfanyabiashara wa madini na pia mchimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo Tanzanite katika machimbo ya Mirerani, Simanjiro Mkoani Manyara amesema Rais Samia Suluhu Hassan anastahili maua yake katika sekta ya madini ambapo katika utawala wake ameweza kujenga jengo kubwa la madini ambapo wafanyabiashara na wanunuzi watalitumia kufanyabiashara na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri mbali kutafuta masoko.
” Mirerani tumejengewa jengo kubwa la zaidi ya bilioni5, hapa kutakuwa na ofisi za madini kwa hiyo wanunuzi wote kutoka pande mbalimbali Duniani na ndani ya nchi watakuwa wakija hapa kununua madini na kuanzia safari zao hapa hapa, ule mnada wa Jaipur India sasa utakuwa hapa, huu sasa unaenda kuwa mji wa madini haswaa,” amesema.
Akizungumzia uchaguzi Mkuu ujao, Nyari amesema Rais Samia hana mpinzani anayeweza kusimama naye jukwaani na kumsemea vibaya, ” Kwa maendeleo yote haya ambayo Mama ameyafanya kweli leo hii kuna mpinzani anayeweza kuja kusema Serikali ya Samia haijafanya kitu? watanzania wameona na nikuhakikishie Mama atapita kwa zaidi ya asilimia 90 uchaguzi ujao,” amesema Nyari.
Amesema kwanza Rais Samia bado ana mipango mizuri katika awamu ijayo ya 2025/2030 baada ya kutangazwa mshindi wa Urais na kwamba yeye binafsi amekuwa na imani mipango hiyo itakamilika kwa muda mfupi sana.
” Watanzania hatuna tunachomdai Rais Samia, na hatuna cha kumlipa kikubwa tumpe kura zetu nyingi itakapofika oktoba mwaka huu, lakini zaidi tunamuombea afya njema na amani ili aliyopanga kuyafanya miaka mitano inayokuja yakamilike bila vikwazo,” Amesema Nyari.
Kuhusu kauli ya upinzani kutaka kugomea uchaguzi, Nyari amesema Watanzania bila kujali itikadi zao ni imani yake kwamba wote wataenda kupiga kura na hakutakuwa na mgomo wowote kwa watanzania.
” Watanzania wako Sawa na tayari kwa uchaguzi Mkuu wa oktoba mwaka huu na wanataka viongozi wao na kama kuna ambao wanaona watashindwa katika uchaguzi huo ni vyema wakaacha kugombea na wakaacha watanzania kutumia haki yao ya kupiga kura na kuchagua viongozi wao,”Amesema.
Akifananisha utawala wa Rais Samia na Marais waliomtangulia, Nyari anasema utawala wa Marais wote waliopita walifanya vizuri lakini alimzungumzia Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ambapo anasema aliweza kuunganisha nchi kwa barabara za lami, kutoa elimu bure kwa watanzania na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia ambao Rais Samia amekuja kuboresha zaidi.
” Marais wote wamefanya vizuri kulingana na wakati wao na kulingana na idadi ya watu walokuwepo, Rais kikwete katika awamu ya nne alifanyakazi kubwa sana, alileta elimu bure kwa watanzania, aliunganisha mikoa kwa lami na kuanzisha diplomasia ya kimataifa, lakini Mama amekuja na gia kubwa zaidi, anahudumia watanzania zaidi ya milioni 60 na wote wana mfuruhia kwa mambo mazuri,” anasema.
Kuhusu kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao kama ilivyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni kutajwa kutaka kugombea, Nyari anasema muda wa kutangaza kama atawania nafasi yoyote katika uchaguzi ujao bado haujafika hivyo hawezi kuzungumzia masuala ya siasa kwa upande huo kwa sasa.
“Kwa utaratibu wa Chama cha mapinduzi ambaye mimi ni miongoni mwa makada wake, kuna utaratibu tunatakiwa kuufuata na ukizingatia majimbo karibu yote bado yana wabunge tena wanatokana na CCM haturuhusiwi kutangaza chochote hadi muda utakapofika,” amesema.
Amesema kwa sasa chama cha Mapinduzi kupitia mamlaka zake kimetangaza wagombea pekee wa nafasi za Urais Tanzania ambapo wagombea ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza Dkt Emmanuel Nchimbi na Zanzibar ni Dkt. Hassan Mwinyi.