MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira amesema kuna baadhi ya watu wanaotaka kugombea ubunge wameanza kunyemelea majimbo kwa kuvunja maadili.
Wasira ameeleza hayo Machi 24, 2025 wilayani Ngara mkoani Kagera alipokuwa akizungumza na wana CCM pamoja na wananchi katika kikao cha ndani cha Chama hicho ambapo ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wanaotaka ubunge pamoja na wabunge waliopo kufuata maadili.
“Mimi ni Makamu Mwenyekiti na kazi yangu mojawapo ni kusimamia maadili sasa watu wanaotaka ubunge wameanza kunyemelea na wananyelea kwa kuvunja maadili. Tunataka wajumbe mpige kura mkiwa watu huru muiambie CCM tukimsimamisha huyu tunashinda bila tabu kama tutakavyoshinda tukiwa na Dk.Samia.”
Akieleza zaidi amesema CCM inataka wajumbe hao kupitisha jina moja kati ya majina matatu ya wagombea na huyo atakayepitishwa watu wanasema kama ni huyu sawasawa.
“Lakini wale wanaotaka ubunge nina habari zao, wameanza kuvuruga maadili, wanataka mpige kura kwa hela wanazowapa, na biblia inasema rushwa inapofusha, maana yake ni kwamba ukiona mtu amejaa kijani lakini ukipewa rushwa unasema hiyo sio kijani hiyo ni bluu.
“Rushwa imekwambia hivyo na wewe unang’ang’ania hivyo na unaweza hata ukapigana kwamba ni bluu na huku ni kijani na rushwa ndio inafanya hata upigane kwa sababu rushwa imepofusha macho yakio, na hapa mmeshaanza na wengine wameshasogezewa elfu kumi kumi.