Na Seif Mangwangi, Arusha
KAMATI ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya Umma (PIC), imeshangazwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Oloirieni Arusha maarufu kama PPF.
Kutokana na mandhari mazuri ulipojengwa mradi huo pamoja na miundombinu ya kisasa ikiwemo barabara za lami, bustani na miti wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati Augustine Vuma wameufananisha mradi huo sawa na mazingira ya miji iliyoko katika majiji makubwa ya New York Marekani, London nchini Uingereza na Johanessburg Afrika kusini.
Wakizungumza leo Machi 26, 2025 walipotembelea mradi huo, wajumbe wa kamati hiyo wamesema wameridhishwa na uwekezaji katika eneo hilo na uongozi mzima ukiongozwa na mkurugenzi mtendaji wanastahili pongezi kubwa.
“Tumetembelea miradi mingi lakini mradi huu hakika ni mzuri sana, ukiwa hapa utafikiri uko katika majiji ya London, New York au Afrika Kusini, ni eneo linalovutia hasa kwa barabara na miti mliyopanda kumependeza sana, kamati nzima tunasema tumeridhishwa lakini angalieni thamani ya kodi kwa kuwa hata kama ni bei ya ghali lakini huku wanaishi matajiri lazima walipe ghali,”amesema Mbunge Augustine
Katika taarifa yake kwa kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Abdulrazaq Abdu amesema mradi huo wenye nyumba 90 zenye hadhi mbalimbali ikiwemo nyumba za ghorofa, eneo la wapangaji la kupumzikia, eneo la kufanyia michezo mbalimbali, mgahawa, eneo la ndani la kufanyia mazoezi(Gyme), na maduka makubwa umeanza kurejesha faida kwa mfuko huo.
Amesema mradi huo uliojengwa na uliokuwa mfuko wa PPF kabla ya mifuko kuunganishwa na kuwa PSSSF katika eneo la mita za mraba 99,000 ulitumia gharama ya shilingi bilioni 13.29 na ilipofika mwaka 2012 gharama zote za mradi huo zilirejea na hivyo kuanzia mwaka huo mradi huo umekuwa ukijiendesha kwa faida.
Abdu amesema kwa mujibu wa tathmini ya thamani ya mradi huo hadi kufikia Juni mwaka 2024 mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 29 na kufanya kuwa moja ya miradi yenye faida kupitia mfuko huo.
“ Mapato yanayotokana na upangishaji kwa sasa ni wastani wa shilingi bilioni 1.6 kwa mwaka, bei ya kodi ya pango inaanzia shilingi 1,080,000 kwa mwezi hadi milioni 2700,000 kwa mwezi kutegemea aina ya nyumba, maeneo ya biashara ni kati ya shilingi 10,800 hadi 16,200 kwa mita za mradi kwa mwezi,”amesema.
Mkurugenzi Abdu amesema kuanzia mwaka 2017 mfuko ulianza kufanya matengenezo makubwa ya maboresho ya nyumba hizo yakihusisha ukarabati wa mifumo ya bomba, umeme, samani za bafuni na jikoni na upakaji wa rangi.
“Hadi sasa jumla ya nyumba 67 zimekarabatiwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5 awamu ya mwisho ya ukarabati inahusisha nyumba 23 inaendelea ambapo inatarajiwa kukamilika mwezi juni 2025 na baada ya hapo nyumba zote zitakuwa na wapangaji asilimia 100,”amesema.
Wakichangia baada kutembelea eneo la mradi, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Fratei Massay Mbunge wa jimbo la MbuluVijijini, amesema mradi huo ni mafanikio makubwa kwa mfuko lakini pia kwa serikali ya Chama cha mapinduzi.
Mbunge huyo ametoa wito kwa mashirika na taasisi zingine za Serikali kuiga mfano wa mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama hiyo ya nyumba za kupanga hususani kwenye maeneo ya miji mikubwa kwa kuwa gharama zake ni rahisi kurejea na kuanza kupata faida.