Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania(NBAA) imeendelea kutoa elimu na kujenga ufahamu juu ya Taaaluma ya Uhasibu kwa wanafunzi wa vyuo na shule mbalimbali za sekondari nchini.
Kwa kipindi hiki NBAA imetembelea wilaya ya Muheza mkoani Tanga ikiwa na lengo la kuwajengea ufahamu wanafunzi kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Bodi hiyo.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo Afisa Masoko na Mawasiliano Mwandamizi wa NBAA, Magreth Kageya amesema lengo la ziara hizo ni kuwahamasisha wanafunzi walioko shuleni hasa shule za Sekondari na vyuoni kupenda na kusoma masomo ya Uhasibu.
Pia amesema si kila aliyesomea uhasibu anaweza kufanya kazi za kihasibu bali inabidi kufanya mitihani ya Bodi hiyo ili kupewa cheti cha kitaaluma ili aweze kutambulika kama Mhasibu na kuweza kufanya kazi nje na ndani ya nchi.
“Kwasasa NBAA inatoa kozi nyingine za muda mfupi kama vile Cheti na Diploma ya IPSAS pamoja na “Professional Diploma in Internal Auditing – PDIA” kozi ambayo inatoa misingi kwa mtu yeyote anayefanya au anatamani kufanya kazi za ukaguzi wa ndani.” amesema Kageya
Naye Mfanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Sawa Ngendabanka ametoa elimu kwa wanafunzi kuhusu hatua wanazoweza kupitia ili kuweza kufikia kwenye hatua ya kupata cheti cha Taaluma yaani CPA.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni ATEC I na ATEC II kwa ngazi ya watunza vitabu na Foundation, Intermidiate na Final kwa ngazi ya Taaluma.
Pia amewataka wanafunzi kuzingatia masomo ya hesabu na kiingereza kwani ndio msingi wa taaluma ya Uhasibu.

Afisa Masoko na Mawasiliano Mwandamizi wa NBAA, Magreth Kageya akitoa elimu kuhusu kazi zinazofanywa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ngomeni iliyopo Muheza mkoani Tanga.
Mwalimu wa Taaluma wa shule ya Sekondari ya Ngomeni akiwatambulisha na kuwakaribisha wafanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kuwahamasisha wanafunzi hao kujiunga na masomo ya Uhasibu watakapomaliza masomo yao ya Sekondari.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ngomeni wakifuatilia elimu iliyokuwa inatolewa na wafanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) waliofika shuleni hapo Muheza mkoani Tanga.