Na Ashrack Miraji Michuzi Tv
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amewaonya wananchi wanaojitokeza kudai umiliki wa eneo linalojengwa Kituo cha Afya Vunta baada ya kuona kwamba serikali imefungua fedha za mradi na ujenzi umeanza. Amesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kughushi nyaraka za umiliki wa ardhi hiyo.
Mhe. Kasilda alitoa onyo hilo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya, akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, baada ya kudaiwa kutokea kwa malalamiko ya mwananchi mmoja ambaye alijitokeza kudai umiliki wa eneo hilo. Aliagiza Halmashauri na Serikali ya Kijiji kuwasilisha uthibitisho wa umiliki wa eneo hilo, na kuongeza kuwa, ikiwa itabainika kuwa Halmashauri ilifanya makosa katika taratibu za umiliki, basi mwananchi husika atafidiwa kwa mujibu wa sheria.
“Eneo hili lilitolewa na wazee wetu ili serikai ijenge kituo cha afya na wananchi wapate huduma karibu. Sasa mnapokuja kusema eneo lilikuwa la mababu zenu, hili sio sawa. Eneo hili lilikuwa na migogoro na tulishautatua muda mrefu. Halmashauri na Serikali ya Kijiji fuatilieni kwa nini mwananchi huyo ajitokeze leo, baada ya mradi kuanza kutekelezwa. Naomba mtu yeyote asiguse eneo la serikali,” alisema Mhe. Kasilda.
Aidha, Mhe. Kasilda aliwasihi wananchi kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, akisisitiza kwamba wao ndio wanufaika wakuu wa mradi huu. Aliweka wazi kuwa ushirikiano wao utasaidia kukamilika kwa ujenzi kwa haraka na kwa viwango vinavyohitajika, na hivyo kuwa mkombozi kwao kwa kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Pamoja na hayo, Mhe. Kasilda ameielekeza Halmashauri kuhakikisha kuwa inatengeneza mipaka rasmi kwenye maeneo ya serikali ambayo yanatolewa na wananchi kwa ajili ya miradi, ili kuepusha migogoro ya baadaye kuhusu umiliki wa ardhi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Programu ya Tanzania Maternal and Child Health Investment Program (TMCHIP), ikiwa na lengo la kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto vijijini. Dkt. Alexander alisisitiza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kuondoa changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Vunta, John Stephan, kwa niaba ya wananchi, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuanzisha ujenzi wa kituo hicho. Amesema kuwa awali, hawakutegemea kuwa eneo lao, lenye mandhari ya milima, lingeweza kupata kituo cha afya.
Ujenzi wa Kituo cha Afya Vunta ulianza mwezi Februari mwaka huu, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti. Hadi sasa, zaidi ya shilingi milioni 629 zimeshatolewa na ujenzi unaendelea.