Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, ndugu Ostadh Rajabu Abdullaman, amesisitiza umuhimu wa kuitunza amani katika taifa letu, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha mshikamano na umoja wakati wa kusherehekea Sikukuu ya Eid Elfitr.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati akitoa salamu za Eid kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu, Ostadh Abdullaman alisema kuwa ni muhimu kwa watu wa Mkoa wa Tanga kusherehekea kwa upendo na kuzuia vitendo vya kuvunja amani. “Tusherekee kwa upendo na mshikamano, na tuendelee kuitunza amani katika mkoa wetu,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka watu wote wenye viashiria vya kuvunja amani katika mkoa wa Tanga kujizuia na kutokubali kuingizwa katika siasa za kuleta mfarakano. “Hatufai kuchezewa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga kinatoa wito wa kutunza amani, na hatukubali kuvurugwa na watu wanaopanga kuvunja utulivu wetu,” aliongeza.
Pamoja na hayo, Mhe. Ostadh Abdullaman alitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake kubwa za kulinda amani nchini. “Rais Dkt. Samia anajitahidi kwa dhati kuhakikisha kuwa amani inadumishwa. Hatufai kuchezea amani tunayokuwa nayo, kwani madhara yake ni makubwa,” alisema.
Ostadh Abdullaman alifafanua kuwa Watanzania hawatambui umuhimu wa amani hadi itakapopotea. “Ni wakati huu tu tutakapokuwa na upungufu wa amani ndipo tutatambua thamani yake,” alisisitiza.
Vilevile, alitowa wito kwa wanasiasa wanaojiandaa kufanya siasa mkoani Tanga kuwa waangalifu na kuhakikisha wanahakikisha amani inadumishwa. “Tanga siyo mahala pa vurugu. Wanasiasa wanaokuja kufanya siasa hapa tunawasisitiza kuzingatia amani,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian, kwa juhudi zake za kutatua migogoro na kudumisha amani katika mkoa huo. “Serikali ya Mkoa wa Tanga inatumia busara na hekima kutafuta amani, na tunaomba wananchi waungane na serikali katika juhudi hizi,” alisema.
Mwisho, Ostadh Abdullaman alitoa wito kwa watu wenye uwezo kusaidia wagonjwa na mayatima katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Eid Elfitr, ili kila mmoja aweze kusherehekea kwa furaha. “Tuonyeshe huruma kwa wale wanaohitaji msaada katika kipindi hiki cha sherehe,” alimalizia.