
Songea, Tanzania — Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema hakuna sababu ya kuilazimisha CHADEMA au chama chochote kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025, akisisitiza kuwa ni haki ya chama kuamua kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo. Amesema ni kosa kubwa kukilazimisha chama cha siasa kushiriki uchaguzi huku akibainisha hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuzuia Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) unaofanyika Songea Mjini mkoani Ruvuma leo, Dk.Nchimbi ametumia nafasi hiyo kuzungumza kwa sauti ya utulivu lakini iliyobeba ujumbe mzito, amesema uchaguzi mkuu ni matakwa ya kikatiba ambayo hayawezi kusimamishwa na mtu yeyote, hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tumekuwa tukifanya hivyo tangu mwaka 1961 ,kila baada ya miaka mitano Uchaguzi Mkuu. Ukifika mwaka wa uchaguzi mkuu hakuna raia yeyote anayeweza kuzuia uchaguzi “Hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawezi, hata Makamu wa Rais hawezi, Waziri Mkuu hawezi kulitamkia Taifa kuzuia uchaguzi mkuu. “Kwasababu hilo ni takwa la kikatiba ,ninataka niwahakikishie sio wahariri bali Watanzania wote kuwa uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais mwaka 2025 utafanyika.”
Dk.Nchimbi pia amesema pamoja na haki ya kuchagua na kuchaguliwa ni kosa kubwa kukilazimisha chama kingine cha siasa kuingia kwenye uchaguzi.