
Mbinu na nia bora za ufundishaji kwa wanafunzi zimetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha kupandisha ufaulu na kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Geita, Constantine Molandi, wakati akihutubia mahafali ya tatu ya kidato cha sita katika shule ya sekondari Shantamine iliyopo Kata ya Mtakuja, Wilaya ya Geita. Amesema mafanikio yanayoshuhudiwa katika shule hiyo ni matokeo ya ubunifu na juhudi za walimu katika kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na mitihani ya kitaifa.
Kwa upande wake, kupitia risala ya wanafunzi wa kidato cha sita, mhitimu Joyce Reuben alieleza kuwa walimu wamekuwa msaada mkubwa kwao, hasa katika maandalizi ya mitihani ya majaribio, jambo lililosaidia kuongeza kiwango chao cha ufaulu.
Naye Mkuu wa shule ya Shantamine, Swila Kakila, amewataka wazazi kuwa makini na matumizi ya simu za mkononi kwa watoto, akieleza kuwa simu hizo mara nyingi zimekuwa chanzo cha kuporomoka kwa maadili na kushuka kwa ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi.
Baadhi ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo, Maria Joseph na Yohana Mathias walitoa maoni yao, wakieleza kuridhishwa kwao na maendeleo ya shule hiyo pamoja na nidhamu inayojengwa kwa wanafunzi.
Mahafali hayo yameacha ujumbe mzito kwa jamii, wazazi na wadau wa elimu juu ya umuhimu wa ushirikiano katika kuinua kiwango cha taaluma. Ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi na wazazi umebainika kuwa nguzo kuu ya mafanikio yanayoshuhudiwa katika shule ya Shantamine. Ni mfano hai unaoonyesha kuwa mbinu bora za ufundishaji, malezi yenye nidhamu, na mazingira bora ya kujifunzia ni silaha madhubuti za kuandaa kizazi chenye maarifa, maadili na uwezo wa kushindana kitaifa.