Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Kizito Mhagama, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge Wawakilishi wa umoja wa Mabunge Duniani kutoka Tanzania, ameongoza msafara wa Wabunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 150 wa Mabunge Duniani (IPU) unaoendelea mjini Kashkenti, Uzbekistan, kuanzia Aprili 5 mpaka 9, 2025.
Katika mkutano huu, Mhagama ameonyesha juhudi za Bunge la Tanzania katika kuisimamia serikali na kuhakikisha kwamba inatekeleza majukumu yake kikamilifu, hasa katika nyanja za maendeleo na haki za binadamu.
Mkutano huo unazungumzia nafasi ya Mabunge katika kupigania maendeleo na haki za jamii (Social Development and Justice), ambapo Bunge la Tanzania limekuwa na nafasi muhimu katika kuhamasisha na kutunga sheria zinazolenga kuboresha hali ya maisha ya wananchi.
Mhagama ameelezea hatua muhimu ambazo Tanzania imechukua katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na haki za binadamu, akisisitiza umuhimu wa Mabunge duniani kushirikiana ili kufikia malengo ya pamoja ya maendeleo endelevu.
Huu ni mkutano wa kihistoria ambao umeipa Tanzania fursa ya kuonyesha mchango wake katika masuala haya ya kimsingi, huku ikiendelea kujenga mifumo bora ya utawala inayozingatia haki na maendeleo ya wananchi wake.